Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA Musa Nassoro Kuji amesema kuwa
hakuna eneo korofi la barabara litakalosalia bila kukarabatiwa ndani ya Hifadhi
ya Taifa Serengeti ili kutatua changamoto zilizojitokeza hivi karibuni za
kuharibika kwa miundombinu hiyo kulikosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea
kunyesha nchini na nchi jirani na kuleta adha kwa watalii.
Kamishna huyo anayesimamia Hifadhi za Taifa 21 nchini
ameyasema hayo jana Februari 08, 2024 wakati akifuatilia maagizo yake
aliyoyatoa Januari 26, 2024 kwa menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti ya
kukarabati maeneo korofi ili kuondoa adha itokanayo na kuharibika wa barabara
kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.
“Tunatambua umuhimu wa barabara katika Hifadhi za Taifa
ikiwemo hii ya Serengeti ambapo hivi sasa hali ya barabara zetu inaendelea
kuimarika na tumehakikisha tunaweka nguvu kubwa ili kufikia maeneo yote korofi
na kwa kasi tuliyonayo tumebakiza maeneo machache tu ambayo ukarabati wake
haujakamilika ila unaendelea na tunaimani katika kipindi kifupi kijacho
ukarabati huu utakamilika".
Aidha, Kamishna Kuji alimshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mitambo mbalimbali ya
ujenzi ambayo imesaidia kurahisisha shughuli za ujenzi na ukarabati wa
miundombinu hiyo pindi inapoharibika.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia
miundombinu Mhandisi Dkt. Richard Matolo alieleza kuwa licha ya ukarabati huu
tunaoufanya, bado TANAPA ina mpango endelevu wa kuziboresha barabara hizi kwa
kuziinua juu ili kuruhusu mtiririko wa maji kutoziharibu barabara hizi hususani
nyakati za mvua nyingi.
Mhandisi Dkt. Matolo alisema, “Tumeanza kukarabati maeneo korofi kwa kufukia
mashimo, kuweka mitaro ya kutiririsha
maji barabarani lakini bado tuna mpango wa muda mrefu wa kumaliza kabisa
changamoto ya barabara zetu kwa kuziinua na kuziwekea tabaka gumu litakalodumu
kwa muda mrefu bila kuharibiwa na mvua.”
Aidha, Kamishna Matolo aliongeza kuwa, "Tutaanza
utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya
Seronara - Naabi - mpaka Golini yenye urefu wa kilometa 68 hivi karibuni,
ambapo ujenzi huo utahusisha kujaza kifusi kwa ajili ya kuinua barabara, ujenzi
wa vivuko, uchimbaji wa mitaro ya kupitisha maji na kuweka tabaka gumu
almaarufu "Gravel Wearing Course".
TANAPA inaendelea na ujenzi pamoja na ukarabati wa miundombinu ya barabara zilizoharibiwa na mvua ziweze kupitika vizuri licha ya uwepo wa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Na. Jacob Kasiri- Serengeti
0 Maoni