Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka
Biteko ameuagiza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kuhakikisha
Zahanati ya Kijiji cha Mkangwe, iliyounganishiwa umeme wa REA inaanza kazi mara
moja.
Dkt. Biteko ametoa maagizo hayo jana wakati akizungumza na
wananchi baada ya kuwasha umeme katika Zahanati hiyo.
“Umeme tayari tumewasha, kwahivyo hakuna haja ya kusubiri.
Naagiza Zahanati hii ianze kazi Jumatatu ijayo (Februari 26) ili wananchi
wapate huduma za afya kama Serikali ilivyodhamiria,” amesisitiza.
Aidha, Dkt. Biteko amewaagiza Wakandarasi wanaotekeleza
miradi ya umeme vijijini nchini kote kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati ili
Serikali iendeleze miradi hiyo katika maeneo mengine ambayo hayajafikiwa.
Amesema kuwa kadri miradi ya umeme vijijini inavyoendelea
kutekelezwa katika maeneo mbalimbali, kiu ya wananchi ambao hawajafikiwa
inaongezeka hivyo ameiagiza REA kuhakikisha inasimamia suala la ukamilishwaji
miradi hiyo kwa wakati.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya
umeme vijijini kwa Mkoa wa Iringa, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA,
Mhandisi Godfrey Chibulunje amesema kuwa Vijiji vyote 360 vya Mkoa huo, sawa na
asilimia 100 vimepatiwa huduma ya umeme kupitia miradi mbalimbali
inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Ameongeza kuwa, mbali na kufikisha umeme katika vijiji
vyote, REA pia imefikisha nishati hiyo katika vitongoji 1,188 kati ya 1,853
sawa na asilimia 64.11
“Vitongoji vilivyobaki vipo kwenye mpango wa kufikishiwa
huduma ya umeme kupitia miradi ya ujazilizi na miradi ya vitongoji,” amesema
Chibulunje.
Akitoa takwimu za Jimbo la Mufindi Kusini, ambapo ndipo
kilipo kijiji cha Mkangwe, Mhandisi Chibulunje amesema kuwa vijiji vyake vyote
71 sawa na asilimia 100 vimekwishafikishiwa umeme kupitia miradi mbalimbali ya
REA.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na REA Awamu ya Tatu
Mzunguko wa Pili, Mradi wa kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za
Maji pamoja na Mradi wa kupeleka umeme kwenye Vitongoji.
Kuhusu Vitongoji, ameeleza kuwa Jimbo la Mufindi Kusini lina
jumla ya Vitongoji 305 ambapo kati yake, 191 tayari vimekwishapatiwa umeme.
Kwa upande wa gharama zilizotumika kutekeleza miradi ya
umeme katika vijiji vya Jimbo la Mufindi Kusini, amesema kuwa jumla ya shilingi
bilioni 7.6 zimetumika.
Hafla hiyo ya kuwasha umeme imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Vyama vya Siasa na Serikali, wananchi pamoja na Wataalamu kutoka REA na TANESCO.
Na. Veronica Simba- REA
0 Maoni