Apandishwa kizimbani kwa kutokutunza kumbukumbu za dereva wake

 

Paulo Mahuma (59) mkazi wa kijiji cha Isandula Wilaya ya Magu mkoani Mwanza amefikishwa katika Mahakama ya wilaya ya Magu na kusomewa shtaka la kushindwa kutunza kumbukumbu za dereva aliyekuwa amemuajiri kwa shughli ya kuendesha gari lake.

Mahuma amesomewa shtaka hilo leo Februari 16.2024, katika kesi ya trafiki namba 4045/2024, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Magu Erick Kimaro.

Akisoma shtaka hilo Mwendesha Mashtaka wa Serikali Peter Ilole amesema mshtakiwa Paulo Mahuma alikamatwa na Jeshi la Polisi tarehe 13.12.2023 na kufikishwa kituo cha Polisi Magu akiwa mmilki halali wa gari lenye namba ya usajili T.608 DMP aina ya TATA kwa kushindwa kutunza kumbukumbu za dereva wake aliyekimbia mara baada ya kusabaisha ajali kinyume na kifungu 79 na 89 (a) cha sheria ya usalama Barabarani Sura ya 168 marejeo ya mwaka 2002.

Mwendesha mashtaka amesema watu wawili walifariki na wengine kujeruhiwa katika ajali hiyo ambapo gari hilo liliacha njia na kupinduka katika Mto Simiyu.

Taarifa ya ajali hiyo iliyotokea tarehe 13.12.2023 katika kijiji cha Ng'aya, kata ya Sukuma wilaya ya Magu, barabara ya Magu-Bariadi ilitolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa alipotembelea eneo ilipotokea ajali hiyo.

Mshtakiwa ameachiwa huru baada ya kukidhi masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka kwa viongozi wa Serikali za Mitaa na kusaini bondi isiyohamishika yenye thamani ya milioni moja  kwa kila mdhamini na nakala ya kitambulisho cha Taifa (Nida) ama kitambulisho cha mpiga kura kwa kila mmoja.

Hakimu Kimaro ameahilisha shauri hilo hadi Februari 23, 2024 litakapoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kuanza kusomewa hoja za awali.



Chapisha Maoni

0 Maoni