Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia
ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdullah ametoa wito kwa Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania kuendelea kushirikiana na wizara kwa lengo la kupata
uelewa zaidi kuhusu majukumu na miradi inayotekelezwa na wizara.
Bw. Khamis amesema hayo leo Januari 25, 2024 alipokutana na
Kamati ya Wataalam wa Mawasiliano kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania waliofika ofisini kwake kwa lengo la kujifunza masuala mbalimbali ya
mawasiliano.
Bw. Mohammed Khamis Abdullah ameieleza kamati hiyo
iliyooongozwa na Luteni Kanali Lukwaro Mbwambo kuwa wizara kupitia sekta ya
mawasiliano ina miradi tisa ambayo inasimamia utekelezaji wake.
Alisema miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Ujenzi wa Mkongo
wa Taifa, Mradi wa Mfumo wa Anwani za Makazi, Mradi wa Mfumo wa jamii namba,
Mradi wa Usambazaji wa Mawasiliano Vijijini, na Mradi wa Ujenzi wa Data center.
Aidha, miradi mingine ni Mradi wa Kurusha Satelaiti, Mradi
wa Chuo cha TEHAMA, Mradi wa kuendeleza bunifu katika TEHAMA pamoja na mafunzo
kuhusu Teknolojia zinazoibukia katika TEHAMA.
Akitoa salamu kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Luteni Kanali Lukwaro Mbwambo ameishukuru wizara
kwa wasilisho hilo na kuahidi kufanya uchambuzi ili kuona ni kwa kiasi gani
Jeshi litaweza kutumia miradi hiyo kujiimarisha katika eneo la mawasiliano.
Bw. Mohammed Khamis Abdullah ameteua timu ndogo ya Wataalam itayoongozwa na maafisa waandamizi wa wizara ili kuungana na wataalam kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na kuja na mapendekezo ya namna ya kuendelea na ushirikiano huu.
0 Maoni