Waziri wa Maji Mhe. Jumaa
Aweso (Mb) ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma
(DUWASA) kuweka mpango mkakati wa dharura wa kuhakikisha upatikanaji wa huduma
ya majisafi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) inapatikana haraka kwa uhakika
na ubora.
Mhe. Aweso amesema
hayo leo Januari 23,2024 akiwa katika ziara ya kikazi jijini Dodoma
katika Chuo Kikuu cha UDOM na chanzo cha maji cha Iyumbu kufuatilia hali ya
upatikanaji wa maji chuoni hapo, na
ameihakikishia jumuiya ya chuo hicho na
wanachuo kuwa hali ya huduma ya maji itaimarika na kwamba kazi ya
serikali ni kuwapatia wananchi wote huduma ya majisafi.
Mhe. Aweso amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi
Aron Joseph kuhakikisha anaweka mtandao wa maji unaojitegemea ili kutoa huduma
UDOM kutoka chanzo cha maji cha Nzuguni, ambapo Wizara ya Maji itawezesha
utekelezaji wake.
Aidha, ameitaka DUWASA kuongeza upatikanaji wa maji chuoni
hapo kutokana na dharura iliyopo.
Mhe. Aweso katika hatua nyingine ameagiza kuendelea
kufanyika utafiti wa kina katika maeneo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ili
kutambua uwepo wa maji chini ya ardhi.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Lughano Kusiluka amesema bado UDOM ina uhitaji mkubwa wa majisafi upatao lita 2,296,000 zinazohitajika kuweza kuhudumia wanachuo wapatao elfu 33, ambapo kwa sasa chuo hicho kinapata lita 1,172,000 kutoka DUWASA sawa na asilimia 51 kutoka vyanzo vya Mzakwe na Iyumbu.
0 Maoni