Timu ya wataalamu tisa wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) leo tarehe 17/01/2024 wamesafiri kwenda nchini Zambia kwa jili ya kutoa
huduma ya upasuaji wa moyo kwa watoto katika Hospitali ya Taifa ya Moyo ya
nchini humo.
Katika kambi hiyo ya upasuaji ambayo itafanyika kuanzia
tarehe 18/01/2024 hadi tarehe 20/01/2024 wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na
wenzao wa Zambia watafanya upasuaji huo ambao utaenda sambamba na kuwajengea
uwezo na ujuzi wa kazi.
Wataalamu hao ni madaktari bingwa wa watoto, upasuaji wa
moyo, usingizi na wagpnjwa mahututi, maafisa uuguzi wanaohudumia wagonjwa
wanaohitaji uangalizi maalumu na wataalamu wa kuendesha mashine ya kuusaidia
moyo na mapafu kufanya kazi (Heart Lung Machine).
Daktari bingwa mmoja ametangulia nchini Zambia kwaajili ya
kufanya uchunguzi wa moyo kwa watoto ili kubaini watoto ambao wanahitaji
kufanyiwa upasuaji katika kambi hiyo ya matibabu.
Kufanyika kwa kambi hii ya upasuaji wa moyo ni utelelezaji
wa mkataba wa miaka mitatu wa makubaliano baina ya JKCI na Hospitali ya Taifa
ya moyo ya nchini Zambia wa kutibu wagonjwa wa moyo pamoja na kuwajengea uwezo
wataalamu wa afya wa hospitali hiyo wa
jinsi ya kuwatibu wagonjwa wa moyo uliosainiwa
tarehe 20/04/2023 jijini Dar es Salaam.
Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH)
la nchini Israel ndilo lililowezesha kusainiwa kwa mkataba huo pamoja na kufanyika
kwa kambi hiyo ya upasuaji nchini Zambia.
Mwaka 2015 SACH ilianza ushirikiano na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwajengea uwezo wataalamu wa afya kwa kufanya kambi mbalimbali za upasuaji wa moyo kwa watoto na kutoa mafunzo nchini Israel ambapo hadi sasa JKCI imekuwa na uwezo wa kufanya upasuaji wa moyo. Kutokana na wataalamu wa JKCI kuwa na ujuzi wa kutosha katika upasuaji wa moyo kwa watoto SACH imeiunganisha JKCI na nchi ya Zambia ili waweze kuwasimamia ili nao wapate ujuzi huo na kuweza kufanya upasuaji.
0 Maoni