TAWIRI yaanza kuwatoa visukuma mawimbi tembo njia ya msongo wa kV400

 

Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya utafiti wa wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Dkt. Eblate Ernest Mjingo amesema Taasisi  hiyo  imeanza rasmi zoezi la kuwatoa Tembo mikanda ya visukuma  mawimbi  (GPS Collars ) katika  Wilaya za Longido,  Hanang,  Babati, Monduli  ambapo kuna shoroba za wanyamapori  zilizopitiwa na   mradi wa Njia ya Umeme  ya Msongo wa kV 400 wa Kenya - Tanzania  Power  Interconnection Project (KTPIP).

Akizungumza Wilayani  Longido, Dkt.Mjingo  ameeleza kuwa katika Mradi wa KTPIP unaokatiza  maeneo ya Shoroba za wanyamapori  za Tanganyeeti na Laasarack Wilayani Longido, Ushoroba  wa Kwakuchinja Wilayani Babati, Mswakini chini Wilayani Monduli na Pori la akiba la Swagaswaga, TAWIRI imefanya tafiti  na kuishauri Serikali  kupitia TANESCO ili kuwa na uhifadhi  endelevu nchini.

 "Ili kupata taarifa  za kisayansi ,njia mbalimbali za kitafiti  zimeendelea kutumika  katika mradi huu ambapo mwaka 2019 tuliwafunga Tembo 30 GPS Collars katika shoroba hizo  kwa lengo la kufuatilia kama wanyama wataendelea kupita baada ya kutekeleza mradi. Matokeo ya awali  yameonyesha wanyama wameendelea kupita hata baada ya miundombinu kusimikwa   na ufuatiliaji  unaendelea pale umeme utakapowashwa, " amefafanua Dkt. Mjingo.

Mkuu wa Wilaya  ya Longido  Mhe. Marco Ng'umbi, wakati wa kuwatoa Tembo GPS collar Wilayani humo, amesema Serikali  ya  awamu  ya  sita  chini  ya  uongozi  shupavu  wa  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan  inahakikisha kunakuwa na uhifadhi endelevu  nchini, ambapo katika  kuwaletea watanzania maendeleo kupitia miradi ya kimkakati inafanya tathimini ya athari za kimazingira na kijamii ambapo hupata ushauri sahihi wa kisayansi kupitia tafiti.

Naye, Mhandisi John Lazimah kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambaye pia ni Mhandisi mazingira katika Mradi huu wa (KTPIP), amesema mradi huo unaunganisha Nchi za Kenya na Tanzania   unalenga kuunganisha mfumo wa umeme wa  Nchi za Afrika  Mashariki ( Eastern African  Power  Pool) na kuziwezesha nchi hizi kuuziana  umeme, kwa Tanzania mradi unatekelezwa kutoka Singida hadi Namanga kupitia kituo cha kupooza umeme cha Lemugur- kilichopo Kisongo Mkoani Arusha.

Aidha, Mhandisi Lazimah  amebainisha kwamba Tanzania  inaendeleaa kukua kiuchumi kupitia mradi wa KTPIP kwa kuzalisha umeme wa ziada  na kuuza kwa nchi nyingine, Pia kuwa na umeme wa uhakika  kunapokuwa na  uzalishaji mdogo  wa umeme nchini kutokana na sababu zisizo epukika, nchi inaweza kununua kutoka   nchi  nyingine na kuwezesha shughuli za kiuchumi na kijamii zinazotegemea umeme kufanyika bila kuathirika.

Kwa mujibu wa Shirika  la Umeme  Tanzania (TANESCO) mradi huu wa Kenya  -Tanzania Power Interconnection Project unagharimu kiasi cha Dola za kimarekani 258 Milioni na unatarajiwa kukamilika mapema  mwaka huu.



Chapisha Maoni

0 Maoni