Kundi lenye kaya 72 wananchi 515 na mifugo 2,206 limeagwa
leo tarehe 18/01/2024 baada ya kujiandikisha na kuamua kuhama kwa hiyari kutoka
katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera handeni Mkoani
Tanga.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi hilo, meneja wa mradi
wa kuhamisha wananchi waishio ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Uhifadhi Fedes Mdala
ameeleza kuwa baada ya kundi hili kuhama leo inafikisha jumla ya kaya 749 zenye
watu 4,337 na mifugo 19,915 ambayo tayari zimehama ndani ya hifadhi kwenda
maeneo yaliyopangwa na serikali pamoja na maeneo mengine ambayo wananchi
wamechagua.
Kamishna wa Uhifadhi NCAA Richard Kiiza ameeleza kuwa kundi
la awamu hii ndio kubwa zaidi kuondoka tangu kuanza utekelezaji wa zoezi hili
na kuongeza kuwa kadri ujenzi wa Nyumba za makazi unavyoendelea Kijiji cha
Msomera, kitwai na Saunyi idadi ya wananchi wanaojiandikisha kuhama kwa hiari
imeendelea kuongezeka ambapo hadi sasa zaidi ya kaya 1,070 zimeshajiandikisha
kuhama na zoezi la uhamasishaji na uelimishaji linaendelea.
Kamishna Kiiza ameongeza kuwa zoezi la ujenzi wa Nyumba
5,000 katika Kijiji cha Msomera, Saunyi na Kitwai linaendeela chini ya SUMA JKT
na tayari zaidi ya nyumba 360 zimeshakamilika na nyumba zingine zaidi ya 2,000
na nyumba nyingine ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Kiiza amewahimiza wananchi walioagwa leo kuendelea kuwa
mabalozi wa kuwahimiza wananchi waliobaki kujiandikisha kuhama kwa hiari ili
wanufaike na Maisha bora yaliyoandaliwa na Serikali nje ya Hifadhi.
Akiwaaga wananchi hao Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali
Wilson Sakulo ameeleza kuwa wananchi wanaohama kwa hiyari wanapewa stahiki zao
zote za msingi ikiwepo nyumba yenye hati kwenye eneo la ukubwa wa ekari 2.5,
shamba la kulima la ekari tano, huduma za maji, shule, afya, barabara, mabwawa,
majosho, minada, umeme na huduma za mawasiliano na kupata uhuru wa kufanya
shughuli za kilimo na kuishi Maisha huru tofauti na hifadhini.
Kanali Sakulo ameelekeza uongozi wa NCAA kuendelea kutoa
elimu, uhamasishaji na uandikishaji kwa wananchi walio tayari kuhama kwa hiari
na kuhakikisha kuwa kila mwananchi aliyejiandikisha kuhama anahamishwa kwa
wakati, kupata stahiki zake zote na kuhakikisha wananchi wanaohama hawarudi
tena maeneo ambayo wameshahama kwa kuwa Serikali yetu imeshawajengea mazingira
wezeshi yenye huduma zote muhimu za kijamii.
Mmoja ya wananchi aliyehama Petro Tengesi amemshukuru Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kwa wananchi wa Ngorongoro na kuendelea kuwajengea mazingira bora nje ya hifadhi ikiwemo ulipwaji wa stahiki zao za kuhama, kusafirishiwa mizigo yao pamoja naa kuboreshewa huduma za kijamii nje ya hifadhi.
0 Maoni