Katika kuelekea kuadhimisha miaka 62 ya uhuru wa Tanganyika
ifikapo Disemba 9, 2023 zaidi ya watalii 200 wa ndani na nje ya mipaka ya
Tanzania wameanza safari ya kuelekea katika kilele cha Mlima Kilimanjaro
kupitia lango la Marangu.
Katika safari hiyo wamo waheshimiwa mabalozi 11
wanaiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali, akiwaaga watalii hao, Mkuu
wa Wilaya ya Moshi Mjini Mhe. Kisare Makori alisema, "Kupanda kwa
Waheshimiwa mabalozi katika kilele hiki kirefu kuliko vyote barani Afrika kuna manufaa
makubwa kwa Taifa kwani mnatazamwa na kufuatiliwa na mataifa mnayotuwakilisha,
hivyo msisite kurusha tukio zima la (Twenzetu Kileleni), vivutio vya utalii
mtakavyoviona na fursa za uwekezaji zinazopatikana katika hifadhi hii ili
kuvutia watalii na wawekezaji wengi zaidi.
Vilevile, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Makori aliongeza kuwa
Tanzania ina vivutio vingi na vyenye maajabu mengi yanayovutia, hivyo
mnapoviona vivutio na mandhari nzuri ya hifadhi hizi ni rahisi kuvielezea na
kuvinadi tofauti na mtu aliyesoma katika majarida mbalimbali.
Aidha, Mkuu wa Wilaya huyo, pia alikemea vitendo vya
uharibifu wa mazingira unaopelekea kupungua kwa barafu katika kilele cha Mlima
Kilimanjaro alisema, "Nitoe wito kwa Watanzania wanaoishi mwambao wa Pwani
kuwajibika kuhifadhi maeneo yao, kwani yana mchango mkubwa katika uwepo wa
barafu katika Mlima Kilimanjaro".
Amidi wa muda wa Mabalozi Mhe. Maadhi Maalim alilipongeza
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kuendeleza uhifadhi na utalii
katika maeneo linayoyasimamia ukiwemo Mlima Kilimanjaro.
"Tumekuja kujionea wenyewe uzuri wa mlima huu wa
Kilimanjaro na tumedhamilia kufika kileleni ili tutakaposhuka tukayaambie
mataifa tuliyomo fursa gani zipo ili waje kuwekeza na wengine kutalii",
aliongeza Mhe. Balozi Maalim.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini - TANAPA, Jenerali
Mstaafu George Waitara aliwashukuru
waheshimiwa mabalozi na watalii wengine waliojitokeza katika zoezi la
"Twenzetu Kileleni 2023" kwa kuwa wazalendo kupandisha Bendera ya
Taifa katika kilele cha Uhuru ili kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 62 ya Uhuru
wa Tanganyika.
Sambamba na hayo, Jenerali Mst. Waitara alisema kuwa TANAPA
itaendelea kusimamia rasilimali zote zinazopatikana katika Hifadhi za Taifa na
kuimalisha miundombinu wezeshi ili kurahisisha shughuli za utalii na uhifadhi.
Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Kamishna wa Uhifadhi -TANAPA,
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Herman Batiho, alisema kuwa
TANAPA itaendeleza shughuli za uhifadhi wa pamoja utakaosaidia kutunza mazingira
hasa ya ukanda wa Pwani ili kupunguza kasi ya kupungua kwa barafu ya mlima
Kilimanjaro.
Kumekuwepo na utamaduni katika nchi yetu kusherehekea
kumbukizi ya siku ya uhuru wa Tanganyika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Ili kufanikisha tukio hilo adhimu, TANAPA imeruhusu kwa mwaka huu zitumike njia
3 ambazo ni Lemosho, Machame na leo tarehe 05.12.2023 safari ya kukwea jabali
hilo refu kuliko yote barani Afrika limefanyika katika lango la Marangu.
Na. Jacob Kasiri - Kilimanjaro
0 Maoni