Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko
leo tarehe 29 Desemba, 2023 amezindua Zahanati ya Bungoni iliyopo Mtaa wa
Mafuriko Ilala jijini Dar es Salaam na
kuwataka wananchi kutumia fursa ya uwepo
wa huduma ya zahanati hiyo kutumia huduma badala ya kwenda mbali kufuata huduma
za afya, kwani ni dhamira ya Serikali kusogeza huduma kwa wananchi.
"Niwaombe viongozi wenzangu tuliopewa dhamana na Mhe.
Rais kuhakikisha tunawahudumia kwa vitendo wananchi na kuinua hali za wanyonge
kwa kuwapatia huduma bora wanazostahili," alisisitiza Dkt. Biteko.
Aliwataka wananchi wa Ilala kumpa ushirikiano mbunge wao kwa
vitendo na kumpongeza kwa kazi kubwa aliyofanya ya kuleta maendeleo kwa wanachi
wake, na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano wa mbunge huyo kufanikisha
ujenzi wa zahanati hiyo na kukemea wachache wanaojificha kwenye kivuli cha
taratibu kuchelewesha maendeleo.
Ujenzi wa zahanati hiyo ulianza mwezi Februari mwaka huu,
kwa jitihada za wananchi na baadae Serikali na umegharimu kiasi cha shilingi
milioni 351, ukihusisha gharama za ujenzi, samani, dawa na vifaa tiba na
umefadhiliwa na African Relief Agency na Taasisi ya Rahma International kutoka
Kuwait na inamilikiwa kwa asilimia mia moja na Serikali.
Aidha, Dkt. Biteko alipata fursa ya kutembelea jengo hilo
linalohusisha wagonjwa wa nje yani OPD, Kliniki ya Baba, Mama na Mtoto pamoja
na jengo la kujifungulia na kusalimiana na kinamama waliojifungua kwenye
Zahanati hiyo.
Zahanati hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia kata nne
zilizopo wilaya ya Ilala ambazo ni Ilala, Buguruni, Sharifu Shamba, na
Mchikichini wapatao 12,000.
Akizungungumza wakati wa hafla hiyo, mbunge wa Jimbo la
Ilala na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Mussa Azan Zungu amewataka
watendaji kuhakikisha wanatumia vyema fursa za wafadhili wanaokuja kuwekeza
Kwenye sekta ya afya na kuondoa mikwamo inayoweza kuchelewesha maendeleo.
Mhe. Zungu amesema, wilaya ya Ilala inapokea wageni wengi
kwa siku, sambamba na wananchi wenye mahitaji kwenye Sekta ya Afya hivyo uwepo
wa vituo hivi utasaidia kuboresha utoaji wa huduma.
Awali, akitoa taarifa ya mafanikio ya Idara ya Afya kwa Mhe.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji Dkt.
Zaituni Hamza amesema kuwa, wamefanikiwa kujenga jumla ya vituo vipya saba vya
kutolea huduma na kupandisha hadhi zahanati tano kuwa vituo vya afya, hivyo
kufanya jumla ya vituo vya afya kuwa 12.
Aliongeza kuwa kuelekea mwaka wa mama 2025, imekuja na
miradi ya kimkakati ikiwemo uanzishwaji wa Chuo cha Afya cha Kati na Sayansi
Shirikishi hospitali ya wilaya ya Kivule ambapo jengo la kwanza tayari
limeshapauliwa, lengo ni kuunga mkono azma na dhamira ya Mheshimiwa Rais
kuwaletea maendeleo karibu wananchi wake.
Aidha, Dkt. Zaituni alimshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kuongeza bajeti kwa Wizara ya Afya hususan upatikanaji wa dawa na vigaa tiba kutoka asilimia 90.1 hadi kufikia asilimia 94 na kumuahidi Mheshimiwa Rais kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Ilala Mhe. Mussa Azan Zungu, Mwakilishi wa Balozi wa Kuwait nchini, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mhe. Kumbi la Moto, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Comred. Abas Mtemvu, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, wawakilishi kutoka Wizara ya Afya wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Jiji na Madiwani, viongozi wa CCM kutoka Kata mbalimbali za Wilaya ya Ilala, Jumuiya ya Singasinga nchini na wanachi wa maeneo jirani.
0 Maoni