Wakristo wameambiwa kuwa kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulikuwa
na dhumuni la kuleta amani zaidi kwa mwanadamu ambalo ni tukio lililotokea
miaka zaidi ya 2000 iliyopita, hivyo kwa sherehe ya Noeli kila mwanadamu
anatakiwa kuwa na furaha zaidi na kujipanga upya huku kila mmoja kutimiza
wajibu wake, maana mkombozi amezaliwa.
Hayo yamesemwa katika misa ya mkesha wa Noeli katika Mlima
wa Hija, Desemba 24, 2023 kuamkia Desemba 25, 2023 kando ya viunga vya Parokia
ya Malya, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza na Padri Samsoni Masanja ambaye ni
Paroko wa Parokia hiyo.
“Furaha inayotakiwa na kupokelewa ni ya kuzaliwa Yesu Kristo
na iwe katika mioyo yetu na furaha hiyo idhilike katika kila yeye anayesherekea
sikukuu hii.”
Akiendelea kuhubiri katika misa hiyo Padri Masanja alisema
kuwa Familia ya Yusufu, Maria na Yesu ni Familia Bora na siyo Bora Familia na
ndiyo maana hii ni Familia Takatifu.
Usiku wa mkesha huu wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo kila mmoja
anawajibu wa kuiga mfano huo na kuwa na Familia Bora inayotimiza wajibu wa kila
mwanafamilia.
“Katika injili ya leo tunaambiwa Yesu Kristo alipozaliwa tu
alivishwa mavazi ya kitoto, maana yake wazazi wake walitimiza wajibu wao
ipasavyo. Eee na wewe muumini unatimiza wajibu wako kwa familia yako ? Iwe
katika mavazi, maladhi na chakula? Unakutana na mtoto amevaa vilaka huku tochi
zinamulika, hilo halikubaliki na siyo mafundisho ya Ukristo, wakati baba/mama/
mlezi anavaa vizuri, huku watoto wakiwa na hali mbaya, jamani imani yetu
inatufundisha kutimiza wajibu wetu ipasavyo, iwe kwa baba, mama na hata
watoto.”
Akihubiri usiku huo, Padri huyu kijana aliweza kutoa
mahubiri yaliyowaingia vizuri waamini wake, huku akichanganya Kiswahili na
Kisukuma ambapo kwa hakika kila alipouliza swali iwe kwa Kiswahili au Kisukuma
nao waamini walijibu kwa lugha iliyoulizwa.
Padri Masanja alisema kuwa mwaka mpya wa 2024 umekaribia,
hivyo kama kuna mlei hajajipanga vizuri kwa mwaka kwa mwaka mpya ajipange sasa
na kama hakufanya vizuri kiroho na kimwili kwa mwaka 2023 ajipange vizuri maana
Sikukuu ya Noeli inatukumbusha kutimiza wajibu wetu maana Bwana Wetu Yesu
Kristo amezaliwa.
Misa hiyo iliyoanza saa nne kamili ya usiku ilikamilika majira ya saa 9 usiku, huku watoto kadhaa wakibatizwa na ikuhudhuliwa na viongozi kadhaa wa Hija wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Makatekista na walei, nayo historia ya kuingia Ukristo Tanzania ikisomwa, ambapo Mlima wa Hija hapa Malya Wamisionari wa kwanza walisali Krisimasi ya kwanza wakati Ukristo Ukatoliki ulipokuwa unaingia Jimbo Katoliki la Mwanza mwaka 1878.
Adeladius Makwega- Mwanza
0 Maoni