WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa jamii ya
watanzania kushirikiana na serikali na asasi za kiraia kupambana na matendo ya
ukatili dhidi ya wanawake watoto na wenye ulemavu.
Amesema ili kupata matokeo ya haraka, wanajamii wahusishwe
kuanzia hatua ya upangaji wa mikakati ambayo itatumika kutekeleza afua
zinazohusu jamii yao.
"Namna hii itawawezesha kuzikubali afua hizo na kujiona
kuwa ni sehemu muhimu katika utekelezaji. Wanajamii wasipangiwe bali
washirikishwe kupanga mikakati inayohusu jamii zao."
Ameyasema hayo leo (Jumapili Novemba 26, 2023) Wakati
alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mbio za hisani za
kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, watoto na wenye ulemavu (STOP
GENDER BASED VIOLENCE) zilizohitimishwa katika viwanja vya Forodhani mjini
Zanzibar.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa, ameziagiza Idara na Mashirika ya
Serikali yaimarishe ushirikiano na asasi za kiraia zinazotekeleza afua za
kutokomeza ukatili wa kijinsia.
"Kwa kuwa Serikali zimeshaandaa mipango na mikakati ya
kitaifa, asasi za kiraia zitekeleze shughuli zao kwa kuzingatia mipango hiyo
ili kuharakisha utatuzi wa changamoto za kijinsia."
Mheshima Majaliwa amesema Serikali katika kutekeleza Sheria
ya Msaada wa Kisheria Na. 1 ya mwaka 2017, imewezesha makundi maalum yakiwemo
ya wanawake na watoto kupata haki zao katika vyombo vya usimamizi wa sheria.
"Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikitoa msaada
wa kisheria kwa waathirika wa matukio ya udhalilishaji wa kijinsia ambapo zaidi
ya waathirika 1,700 wamepatiwa msaada wa kisheria na kisaikolijia katika mwaka
2022/2023."
Ameongeza kuwa tayari Serikali imeunda madawati na vituo kwa
ajili ya ulinzi na usalama wa Mmtoto na kutoa huduma za msingi kwa waathitika
wa matukio ya ukatili wa kijinsia.
"Kwa upande wa Tanzania Bara; madawati 1,850 katika
shule za msingi 1,128 na sekondari hadi kufikia Septemba, 2023. Kwa upande wa
elimu ya kati na elimu ya juu madawati 273 yameanzishwa hadi kufikia Juni 2023."
Amesema kwa upande wa Zanzibar jumla ya madawati 40
yameundwa katika vituo vya Polisi ili kuharakisha utoaji huduma kwa waathirika
wa ukatili wa kijinsia. Aidha vituo saba vya kutolea huduma za mahali pamoja
vimeanzishwa Mnazi Mmoja, Makunduchi na Kivunge; Pia Wete, Mkoani, Chake Chake
na Micheweni.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa Wizara, ameziagiza Idara na
Mashirika ya Serikali yaimarishe ushirikiano na asasi za kiraia zinazotekeleza
afua za kutokomeza ukatili wa kijinsia.
"Kwa kuwa Serikali zimeshaandaa mipango na mikakati ya
kitaifa, asasi za kiraia zitekeleze shughuli zao kwa kuzingatia mipango hiyo
ili kuharakisha utatuzi wa changamoto za kijinsia."
Kwa Upande, wake Waziri wa Vijana, Utamaduni na Michezo wa
Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Tabia Maulid Mwita, amesema Serikali ya Rais
Dkt. Hussein Ali Mwinyi imejizatiti katika kuhakikisha inadhibiti vitendo vya
ukatili wa kijinsia.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Asma Foundation, Asma
Ali Mwinyi amesema mbio hizo za hisani zimelenga kukusanya shilingi Milioni 500
ambazo zitatumika kuwawezesha wanawake, watoto na wenye ulemavu waliopata
changamoto za unyanyasaji wa kijinsia.
0 Maoni