Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili umekutana na ujumbe kutoka Jimbo la Shandong nchini China na kujadiliana namna ya kushirikiana ili kuendelea kuboresha huduma za kibingwa na kibobezi sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu.
Ujumbe huo umeongozwa na Kiongozi Mkuu wa Afya wa Jimbo la
Shandong Bi. Ma Lixin umetembelea maeneo mbalimbali ya kutolea huduma ikiwemo
Idara ya Magonjwa ya Dharura kwa upande wa watoto na wodi ya wagonjwa
wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Julieth Magandi amesema kwasasa MNH inapenda
ishirikiane katika maeneo ya ICU, magonjwa ya dharura, upandikizaji wa viungo
ikiwemo ini, uloto na figo.
“Tayari upandikizaji wa figo tunafanya, mpaka sasa tumepandikiza
figo wagonjwa 88 ambapo kati ya hao 81 wamepandikizwa Muhimbili Upanga na
wengine 7 wamepandikizwa Muhimbili Mloganzila. Hata hivyo kwa upande wa
upandikizaji figo tunahitaji kujengewa uwezo katika upasuaji mkubwa zaidi kwani
upandikizaji wa kawaida tunafanya,” amesema Dkt. Magandi.
“Serikali ya Tanzania
inayoongozwa na Mh. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa
katika sekta ya afya kuanzia ngazi ya chini hadi taifa kwa kuweka vifaa tiba
vya kisasa, kwa mfano hapa Muhimbili tunavifaa vya kisasa vya kufanyia
uchunguzi na tiba ikiwemo MRI, Angio Suite, Digital X-Ray na CT-Scan pamoja na
vingine vingi hii yote ni kuhakikisha huduma za kibingwa na kibobezi
zinapatikana hapa hapa nchini,” amefafanua Dkt. Magandi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Tiba Asili na muwakilishi
kutoka Wizara ya Afya Dkt. Vumilia Luggyle amesema Tanzania imepiga hatua
kwenye utalii tiba ambapo inahudumia watu kutoka mataifa mbalimbali Afrika
ikiwemo Zambia, Kenya, Zimbabwe, Malawi, Uganda hivyo kuna umuhimu kwa nchi
hizi mbili kushirikiana.
Kwa Upande wake Kiongozi Mkuu Sekta ya Afya Jimbo la
Shandong Bi. Ma Lixin amefurahishwa na namna ambavyo Muhimbili imepiga hatua
katika utoaji wa huduma za fya hususani za kibingwa na kibobezi na kuahidi
kushirikiana ili kuendelelea kuleta matokeo chanja katika sekta ya afya.
0 Maoni