Baadhi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa kuweka magoti na nyonga bandia katika kambi maalumu inayoendelea Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila wameanza kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya afya zao kuimarika.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo leo,
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji MNH-Mloganzila Dkt. Godlove Mfuko
ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji amesema kuruhusiwa kwa wagonjwa hao
kunadhihirisha namna Mloganzila ilivyokidhi viwango vya kimataifa vya kufanya
aina hiyo ya upasuaji.
“Kwa viwango vya kimataifa mtu aliyefanyiwa aina hii ya
upasuaji kama hakuna dharura yoyote huwa ni siku tatu hadi tano, kwa hiyo na
sisi tunakwenda na viwango hivyo ambapo wagonjwa walifanyiwa jumatatu leo
wanaruhusiwa.”
Dkt. Mfuko amebainisha kuwa mbali na kupata wagonjwa kutoka
karibia mikoa yote ya Tanzania, pia alipatikana mgonjwa kutoka Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), jambo ambalo linaonyesha kuwa kambi siyo tu
imenufaisha watanzania bali hata raia kutoka nchi ya kigeni.
Kwa upande wake kiongozi wa kambi hiyo Prof. Mamoun Gadir
kutoka Hospitali ya Queen Elizabeth nchini Uingereza amesema kuwa mpangilio na
muundo wa hospitali ya Mloganzila hauna tofauti za hospitali za nchi
zilizoendelea na kwamba wataalamu wanayo maarifa ya msingi hivyo wakiongezewa
maarifa za ziada kidogo tu wanaweza kuwa wabobezi.
Aidha ameshauri Hospitali ya Mloganzila kuwa kituo maalumu
cha kutoa matibabu ya ngonya na magoti.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Nyonga na
Magoti MNH-Mloganzila Dkt. Shilekilwa Makira amebainisha sababu mbalimbali
zinazopelekea maradhi ya nyonga na magoti kuwa ni pamoja na umri mkubwa,
maradhi ya Selimundu, Pumu ya Mifupa na Ajali.
Amesema kuwa kambi hiyo mbali na kutoa huduma pia imetoa
fursa kwa wataalamu kutoka hospitali za Temeke RRH, CCBRT na Hospitali ya Rufaa
ya Kanda ya Mbeya (MZRH) kujifunza, pia ametoa shukrani kwa wataalamu wa
Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kushiriki kuwajengea uwezo.
“Baada ya kambi kuisha utaratibu wa matibabu kwa watu wenye
changamoto za nyonga na magoti utaendelea kama kawaida ambapo tutawaona katika
kliniki zetu na kama wataonyesha wanahitaji upasuaji tutawafanyia,” amesema
Dkt. Makira.
0 Maoni