Wimbi la uingizaji wa mifugo
unaofanywa na wafugaji wasioitakia mema nchi yetu ulioanza kushika kasi hivi
karibuni, umegubikwa na siri nzito inayotarajia kuua soko la utalii ulianza
kushika kasi ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha na Nyanda za Juu Kusini kwa ujumla.
Doria iliyofanyika tarehe
17.11.2023 kwa kutumia Helikopta ndani ya hifadhi hiyo imekamata mifugo 812
wakiwemo kondoo 759, ngombe 53 na kubaini mifugo mingine mingi ikiwa pembezoni
mwa hifadhi ikirandaranda kusubiri kuingia na kwenda kuharibu Ardhi Oevu ya
Ihefu ambayo ni lulu na chanzo kikuu cha Mto The Great Ruaha.
Ikumbukwe kuwa ikolojia ya
Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa zaidi ya asilimia 75 hutegemea Mto Ruaha Mkuu, hivyo
madhara yoyote yanayosababishwa na mifugo pamoja na kilimo huathiri utiririshaji
wa maji, athari hizo huenda sambamba na kutoweka kwa wanyamapori. Na
wanyamapori wakitoweka hakutakuwa na utalii.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi
wa Uhifadhi, Godwell Meing’ataki - Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha alisema,
"Mifugo inapoingia hifadhini husababisha mnyang’anyano wa malisho na maji
kati mifugo hiyo na wanyamapori, matokeo ya ushindani huo ni uhaba wa malisho
unaopelekea baadhi ya wanyamapori kufa na wengine wenye nguvu na uwezo wa
kutembea umbali mrefu kutafuta eneo mbadala na kujikuta wakivamia makazi ya
watu".
"Mifugo jamii ya
kondoo, ng'ombe na mbuzi wanatabia ya kula eneo moja kwa muda mrefu tofauti na
wanyamapori, wao wana tabia ya kuhamahama. Tabia hii ya kukaa sehemu moja kwa
muda mrefu huathiri ukuaji wa mimea, huleta mmomonyoko wa udongo, ardhi kukosa
rutuba na mvua kubwa zikinyesha hutokea mafuriko. Madhara hayo yote huathiri
Uhifadhi na Utalii", aliongeza Kamishna Meing’ataki.
Mtaalamu wa tiba za
wanyamapori, Afisa Mwandamizi wa Uhifadhi, Isaya Kiwele kutoka Hifadhi ya Taifa
Ruaha, alisema kuwa mifugo inapoingia hifadhini kuna uwezekano mkubwa wa
wanyama hao kuambukizana magonjwa.
"Magonjwa kama Kimeta
na Mafua ya ndege huingizwa hifadhini na mifugo na pia huweza kutolewa
hifadhini na kupelekwa kijijini na mifugo hiyo hiyo iliyotoka hifadhini na kuleta madhara na vifo kwa
jamii", mara nyingi mlipuko wa magonjwa haya huua sana wanyama na binadamu
na kusababisha watalii kutokuja kutalii nchini na kulikosesha Taifa mapato,
alisema Kiwele.
Ikumbukwe kuwa hili ni tukio
la pili ndani ya mwezi huu Novemba la kukamatwa kwa mifugo mingi kiasi hicho,
tukio la kwanza lilitokea tarehe 13 na 14 Novemba, 2023 ambapo ng’ombe 345
walikamatwa wakichunga kinyume cha sheria na trekta moja iliyokuwa ikiendesha
shughuli za kilimo kinyume cha sheria.
Na. Jacob Kasiri- Ruaha
0 Maoni