Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo imesaini mkataba wa makubaliano na Kiwanda cha Dawa cha Kairuki (KPTL) kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa dawa Muhimbili Upanga na Mloganzila.
Mkataba huo umehusisha
maeneo mawili, kuboresha upatikanaji wa dawa ambazo hazipatikani kwa urahisi
kwenye soko ikiwemo zinazotumika katika upandikizaji wa viungo mbalimbali
mwilini kama figo, kongosho pamoja na dawa zenye ujazo mdogo zinazotumika kwa
watoto na wagonjwa wa saratani.
Eneo la pili la makubaliano
ni kuwajengea uwezo wataalamu wa Muhimbili katika uzalishaji wa dawa na namna
ya kuzitumia dawa zinazozalishwa na kiwanda hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema hiyo ni hatua nzuri
kuwepo kwa kiwanda cha dawa ambacho kinamilikiwa na wazawa na kukidhi viwango
vinavyohitajika.
Amefafanua kuwa Muhimbili ni
Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa na kubwa kuliko zote nchini ina vitanda 2,150
ambapo Upanga kuna vitanda 1,550 na Mloganzila kuna vitanda takribani 600 hivyo
inahudumia wagonjwa wengi.
Awali Mkuu wa Idara ya
Famasi Muhimbili, Mfamasia Nelson Faustine amesema wameona umuhimu wa kuingia
makubaliano ya pamoja ili kutatua baadhi ya changamoto na kuongeza ufanisi
katika utendaji hususani kwa upande wa MNH kwani kiwanda hicho kitaweza kuzalisha
bidhaa kutokana na mahitaji.
“Tuliwafuata kutokana kuwepo
kwa changamoto ya upatikanaji wa baadhi ya dawa kwenye soko hususani
zinazoendana na huduma za kibobezi, baadaye Kairuki wakatembelea Muhimbili na
kufanya majadiliano, tulikubaliana baadhi ya bidhaa ambazo wanaweza kuzalisha
kwa makubaliano baada ya kupokea oda kutoka Muhimbili’’ ameeleza Mfamasia
Faustine
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Kiwanda cha Dawa cha Kairuki Dkt. Muganyizi Kairuki amesema kiwanda
hicho kimedhamiria kuzalisha bidhaa kulingana na mahitaji yaliyopo na
kuhakikisha mkataba uliosainiwa unakua na tija kwa hospitali.
0 Maoni