TASTA yatoa siri ya kuachana na utegemezi wa mbegu za nje

 

Asilimia kubwa ya mbegu za hybrids zinazotumika nchini zinazalishwa kutoka nje ya nchi hali inayoifanya Tanzania kuchangia kuzalisha ajira katika nchi zinazozalisha mbegu hizo badala ya kuzalisha ajira za ndani.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wafanyabiashara ya Mbegu Tanzania (TASTA), Bw. Bob Baldwin Shuma, ameyasema hayo jana wakati akiongea kwenye mafunzo ya ufahamu wa mbegu zilizoboreshwa kwa wahariri na waandishi wa habari wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

“Mbegu zote za hybrids zinazoletwa kutoka nje haziji tu na wala sio msaada, bali zinanunuliwa kwa fedha za kigeni ndipo mnunuzi aende kununua kama ni Zimbabwe ama Zambia,” alisema Bw. Shuma na kuongeza, “Bado inatakiwa kulipa kodi kadhaa na ndio maana zinauzwa bei ghali, lakini kwa mfano sasa kunauhaba wa dola tafsiri yake ni nini tutakapo kosa dola mbegu zitakosekana, kama hatuzalishi mbegu sisi wenyewe za kutosha kunahatari”.

Amesema amekuwa akijitahidi sana kusaidia kuhakikisha kunakuwa na Sera nzuri, kwani ardhi zipo tena safi, kwa mfano maeneo yatakayotengwa kwa irrigation (kilimo cha umwagiliaji) mbegu za hybrids zizalishwe huko huko.

“Tuna mabonde mazuri ambayo yamezungumzwa yapo, hayo mabonde mimi nina nia ya kuyataja tuyafanya yawe chini ya Serikali lakini yatolewe kwa ajili ya kuzalishia mbegu za hybrids kwa njia ya umwagiliaji,” alisema Bw. Shuma.

Ameeleza kwamba ili kuzalisha mbegu za hybrid sheria ya TOSCI inasema kuzalisha mbegu hizo unatakiwa kuwa na nafasi ya mita 400 huku na mita 400 huku na mtu mwingine asilime mahindi katika eneo hilo.

“Kwa hiyo ardhi tulionayo lazima tuwe za Sera nzuri, kule tunapoenda kununua mbegu za hybrids wamefanya hivyo, sisi tusipofanya hivyo tutaendelea kununua huko mbegu hizo,” alisema Bw. Shuma.

Mafunzo hayo ya siku mbili kuhusu uzalishaji wa mbegu bora za kilimo yaliyomalizika leo yameandaliwa na Brains Incorporated Limited (Media Brains) kwa kushirikiana na Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA).

Chapisha Maoni

0 Maoni