Wataalam wapatao 20 kutoka
Wizara ya Madini na Taasisi zake wameanza rasmi mafunzo ya kuwajengea uwezo wa
masuala mbalimbali ikiwemo utafiti, usalama wa makaa ya mawe pamoja na madini
mengine katika Kituo cha Human Resource Development Center Geology, Minerals
nchini Indonesia.
Mafunzo hayo yanafanyika
ikiwa imepita takribani kipindi cha miezi sita tu baada ya kufanyika mazungumzo
na makubaliano ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali katika Sekta ya Madini
ikiwemo kuwaendeleza watumishi na wataalam mbalimbali kwa lengo la kuwajengea
uwezo katika kumsimamia na kuendeleza rasilimali madini.
Itakumbukwa mnano Mei, 2023
Tanzania kupitia aliyekuwa Waziri wa Madini ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko na Balozi wa Indonesia nchini
Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko walijadili kuhusu kuwekeza katika shughuli za
uchimbaji na ushirikiano kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na
Taasisi ya uchimbaji wa madini ya nchini Indonesia inayoitwa Mining Industry
Indonesia.
Masuala mengine
yaliyojadiliwa katika kikao hicho yalikuwa ni pamoja na fursa za mafunzo ya
shughuli za uchimbaji nchini humo ikiwemo usalama migodini.
Katika siku za awali za
mafunzo hayo, ilielezwa kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Indonesia
umekuwepo tangu mwaka 1955 ambapo Serikali ya Indonesia ilishiriki katika
ukombozi wa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara na hatimaye nchi hiyo kujenga
ubalozi wake jijini Dar es Salaam mwaka 1964. Pia, Serikali ya Tanzania
ilianzisha ubalozi wake mwaka 2022 katika jiji la Jarkata nchini humo.
Aidha, kama ilivyobainishwa
katika Vipaumbele vya Wizara kwa Mwaka Wa Fedha 2023/24, miongoni mwa
vipaumbele hivyo ni kuendeleza Madini Muhimu na Mkakati na kuzijengea uwezo
taasisi zake ziweze kutekeleza majukumu yake. Hivyo, kufanyika kwa mafunzo hayo
kunadhihirisha dhamira ya Wizara kufikia malengo yaliyopangwa.
Aidha, hayo yanajiri ambapo
pia mafunzo mengine kwa watumishi na waatalam wa wizara na taasisi zake
wanaendelea na mafunzo yanayohusu namna ya kupata mitaji katika miradi ya madini
*(Mining Financing)* yanayofanyika jijini Arusha.
Mafunzo hayo yamewezeshwa na
Wizara ya Madini kwa kushirikiana na kampuni ya ASNL Advisory Limited pamoja na
ushirikiano na kampuni za Auramet International LLC na Bankable Tanzania
Limited.
Matokeo yanayotarajiwa ni
kuwawezesha maafisa wa Wizara ya Madini na taasisi zake kuwa na ujuzi stahiki
wa kuchambua, kusimamia na kukagua miradi ya uwekezaji katika sekta na kushauri
namna bora ya kiwezesha miradi hiyo kupata mitaji ya kuwekeza ipasavyo.
0 Maoni