Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Tanzania
inakwenda kuwa kitovu cha Utalii wa Tiba kwa kutoa huduma za afya bora na za
kisasa kwa wagonjwa maalumu wa ndani na wa nje ya nchi.
Waziri Ummy amesema hayo jana baada ya kufungua mradi wa
kliniki mpya ya wagonjwa maalum na wa kimataifa iliyopo katika Taasisi ya Tiba
ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) itakayotoa huduma za kliniki kwa wagonjwa
wa ndani na nje ya nchi.
“Haya tutakayoyashuhudia leo ni matokeo ya uwekezaji mkubwa
ambao Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya katika Sekta ya Afya lakini pia
niwapongeze Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) chini ya Prof. Abel Makubi na
Mwenyekiti wa Bodi Prof. Charles Mkony kwa kazi nzuri na kubwa ya kuokoa maisha
ya Watanzania,” amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amewaomba Watanzania wenye uhitaji wa tiba kwa
haraka (kliniki ya wagonjwa maalum na Wakimataifa) ikiwa ni mtumishi au
mfanyabiashara waende MOI ambapo ndani ya masaa mawili unamaliza kila kitu na
kuendelea na shughuli zako.
Aidha, Waziri Ummy ameitaka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na
Ubongo Muhimbili (MOI) iendeshe kliniki hiyo mpya ya wagonjwa maalum na wa
kimataifa kwa ubia na wawekezaji wengine ili kuboresha zaidi huduma zitolewazo.
“Ni jambo zuri sana mmelianzisha lakini tusije kukwama njiani
hivyo tushirikiane na wadau wengine ili huduma hii iendelee na ni matarajio
yangu kwamba kliniki hii mpya ya wagonjwa maalumu na wagonjwa wa Kimataifa
itakuwa kliniki ya mfano ambayo itakua kivutio kikubwa kwa wagonjwa kutoka
katika Mataifa mbalimbali,” amesema Waziri Ummy.
Amesema, Kutokana na uwekezaji mkubwa katika miundombinu
vifaa tiba na wataalamu, Taasisi ya MOl imefanikiwa kupunguza rufaa za
wagonjuwa kwenda nje ya nchi ambapo hivi sasa 99% ya huduma za mifupa
zinapatikana hapa nchini na 97% ya huduma za kibingwa za Ubongo, Mgongo na
Mishipa ya Fahamu zinapatikana hapa chini.
Pia, Waziri Ummy ametoa maelekezo kwa Hospitali nyingine
kuwa na huduma za haraka kwa kuwa Watanzania wanataka huduma za haraka na
zilizobora kwa kuzingatia Weledi, Maadili na Taaluma wakati wa kumhudumia
mgonjwa kwa kuanza na mapokezi mazuri.
Waziri Ummy amewataka Watanzania kuzingatia ulaji bora
ikiwemo kupunguza matumizi ya sukari nyingi, chumvi nyingi pamoja na mafuta
mengi ili kuepuka Magonjwa Yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la juu la Damu
(Presha) na Kisukari kwa kuwa magonjwa hayo yamekuwa yakiongezeka Tanzania.
Mwisho, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza
kilio cha Watanzania na kuboreha huduma za Afya ikiwemo kutoa fedha kwaajili ya
majengo, vifaa na vifaa tiba na Sasa tunakwenda kuwa kitovu cha Tiba Utalii.
0 Maoni