Waziri wa Fedha Mhe. Dkt.
Mwigulu Nchemba (Mb) amesema kuwa Serikali inatarajia kukusanya na kutumia
jumla ya shilingi tilioni 47.424 katika mwaka 2024/2025.
Dkt. Nchemba alisema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi
ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25.
Alisema kuwa makusanyo hayo
yatatokana na vyanzo mbalimbali yakiwemo mapato ya ndani, michango kutoka kwa
Washirika wa Maendeleo na mikopo.
“Mapato ya ndani
yanakadiriwa kuwa shilingi tilioni 34.436 sawa na asilimia 72.6 ya bajeti yote,
Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi tilioni 4.291 sawa na
asilimia 9.0 ya bajeti. Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 6.141
kutoka soko la ndani na shilingi trilioni 2.555 kutoka soko la nje”, alieleza
Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba alisema kuwa
Maoteo ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25 yamezingatia mwenendo wa
ukusanyaji mapato, matarajio ya ukuaji wa uchumi, hali ya uchumi wa dunia
pamoja na mikakati ambayo Serikali inaendelea kuchukua katika kuongeza mapato
ya ndani.
Kuhusu matumizi ya Serikali kwa
mwaka 2024/2025, Dkt. Nchemba alisema Serikali inakadiria kutumia shilingi
tilioni 47.424 kati ya kiasi hicho, deni la Serikali shilingi tilioni 12.101,
mishahara shilingi tilioni 11.774 na uendeshaji wa shughuli za Serikali
shilingi tilioni 8.223.
‘’Matumizi kwa ajili ya
programu na miradi ya maendeleo ni shilingi tilioni 15.325 ikijumuisha ruzuku
ya maendeleo ya Elimu msingi na Sekondari bila ada na Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu,” aliongeza Dkt. Nchemba.
Alifafanua kuwa Makadirio
hayo yamezingatia mahitaji ya kugharamia deni la Serikali, mishahara ya
watumishi wa umma, uendeshaji wa miradi iliyokamilika ikiwemo miundombinu ya
elimu, afya, umeme na maji, ugharamiaji wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na
maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Alisema kuwa misingi
iliyotumika katika kuandaa shabaha za uchumi jumla ni pamoja na kuongezeka kwa
ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za uwekezaji na biashara, kuendelea
kuhimili athari za majanga ya asili na yasiyo ya asili kama ukame, vita,
magonjwa ya mlipuko na mafuriko.
Dkt. Nchemba alieleza
misingi mingine iliyotumika kuandaa shabaha za uchumi jumla ni kuimarika kwa
uchumi wa dunia na utulivu wa bei katika masoko ya fedha na bidhaa, kuendelea
na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuendelea kuimarika kwa utoshelevu wa
chakula nchini na uwepo wa amani, usalama, utawala bora, umoja, utulivu wa
ndani na nchi jirani.
Alisema kuwa kutokana na
uchambuzi huo, Pato Halisi la Taifa linakadiriwa kukua kwa asilimia 5.2 mwaka
2023 na kuongezeka hadi asilimia 5.8 mwaka 2024.
Aidha alisema kuwa Mfumuko
wa bei unatarajiwa kubaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia
3.0 hadi 7.0 katika kipindi cha muda wa kati na Mapato ya kodi kufikia asilimia
12.4 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2024/25 kutoka uwiano halisi wa asilimia 11.9
uliofikiwa mwaka 2022/23.
Mhe. Dkt. Nchemba alieleza
kuwa nakisi ya bajeti ikijumuisha misaada kuwa asilimia 2.2 ya Pato la Taifa
mwaka 2024/25 kutoka matarajio ya asilimia 2.7 ya mwaka 2023/24, kuwa na akiba
ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na
huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4) na Kuimarika kwa
viashiria vya ustawi wa jamii.
Bunge linatarajia kujadili
Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka
2024/25 kwa siku tano kuanzia leo.
0 Maoni