SERIKALI imefanya maboresho
kwenye baadhi ya maeneo katika Sera ya Elimu na Mafunzo ili kutoa elimu ya
ujuzi badala ya elimu ya taaluma pekee ambapo elimu ya lazima itakuwa ya miaka
10 badala ya saba kama ilivyo sasa.
Akitoa taarifa kuhusu
maboresho hayo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema utekelezaji wa maboresho
hayo utaanza mwaka 2027 sambamba na kufuta mtihani wa darasa la saba na badala
yake kuanza kufanyika kwa tathmini darasa la sita kwa ajili ya kujiunga na
elimu ya lazima ya sekondari.
Waziri Mkuu ameyasema hayo
leo jana wakati akitoa taarifa kuhusu kuidhinishwa kwa Sera ya Elimu na Mafunzo
2014, Toleo la 2023 na Mitaala ya Elimu Ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi,
Sekondari na Elimu ya Ualimu kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa
Waziri Mkuu bungeni jijini Dodoma.
Amesema hatua hiyo imefikiwa
baada ya kubainika kwa changamoto mbalimbali zikiwemo, mfumo wa elimu kujikita
zaidi kwenye elimu ya jumla na kukosa fursa za elimu na mafunzo kwa kuzingatia
mahitaji na njia mbalimbali za ujifunzaji kutokidhi kulingana na mazingira.
Ametaja changamoto nyingine
kuwa ni: “Mitaala kutokidhi mahitaji ya mabadiliko ya kiuchumi, kijamii,
kisayansi na kiteknolojia, mfumo usio fanisi wa udhibiti na ithibati ya elimu
na upungufu wa nguvu kazi. Changamoto hizo zilizaa hitaji la kuboresha sera
yetu ya elimu ili kukidhi mahitaji ya sasa na wakati ujao.”
Akifafanua kuhusu maeneo
yaliyoboreshwa kwenye sera hiyo ambayo tarehe ya uzinduzi wake itatangazwa
baadaye, Mheshimiwa Majaliwa amesema: “Sera ya Elimu na Mafunzo imefanyiwa
mabadiliko kwenye maeneo kadhaa ikilinganishwa na sera iliyopita kwa kuongeza
fursa za elimu ya amali (elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi) ambayo
itaanza kutolewa kuanzia kidato cha kwanza.”
Kadhalika, Waziri Mkuu
amesema elimu ya ualimu nayo itaanza kuanza kutolewa kwa wahitimu waliomaliza
kidato cha sita na kuendelea. “Mafunzo ya ualimu yatajumuisha mwaka mmoja wa
mafunzo chini ya uangalizi (internship) baada ya kuhitimu mafunzo tarajali (Pre-service
training).”
Amesema maeneo
yaliyoboreshwa ni katika mfumo wa upimaji na tathmini ambao utazingatia mahiri
zinazohitajika kwa kila ngazi kwa lengo la kuwa na upimaji endelevu na matumizi
ya mbinu mbalimbali za upimaji na tathmini ya maendeleo ya wanafunzi katika
kujifunza.
“Serikali itatoa na
kusimamia matumizi ya kitabu kimoja cha kiada kwa kila somo katika elimu ya
msingi na Sekondari ili kufanikisha upimaji wa matokeo ya ufundishaji na
ujifunzaji unaofanana pia Serikali itaweka utaratibu wa kubaini na kuendeleza
wanafunzi wenye vipaji na vipawa mbalimbali.”
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
amesema Wizara yenye dhamana na elimu ina wajibu wa kuandaa mikakati na mipango
ya sekta ikiwa ni pamoja na kutafuta rasilimali mbalimbali kwa ajili ya
utekelezaji na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa sera hiyo.
Aidha, Waziri Mkuu amesema
Wizara yenye dhamana na TAMISEMI itakuwa na wajibu wa kuratibu na kusimamia
Tawala za Mikoa zenye jukumu la kutekeleza sera kwa kutoa elimu na mafunzo
katika ngazi ya awali, msingi na sekondari na Wizara yenye dhamana na Utumishi
itahusika na upatikanaji wa rasilimali watu.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa
Wizara yenye dhamana na fedha itahusika na utafutaji na upatikanaji wa
rasilimali fedha, Tawala za Mikoa zitasimamia utekelezaji wa sera na miongozo
ya utoaji elimu na mafunzo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Mamlaka za Serikali za
Mitaa zitaendelea na utekelezaji wa sera na hivyo kutoa huduma za elimu ili
kuwafikia walengwa wote. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali itaendelea kushirikiana
na sekta binafsi ikiwemo mashirika ya kidini, mashirika yasiyo ya Serikali na
wadau wengine katika kuboresha upatikanaji na utoaji wa elimu na mafunzo.”
Amesema mgawanyo wa majukumu
utafuata mifumo ya kitaasisi iliyojengwa kisheria na kwa kadri ya utaratibu wa
Serikali. “Wizara yenye dhamana ya elimu pamoja na taasisi zake itaendelea kuwa
na wajibu wa kusimamia, kuratibu na kuimarisha upatikanaji na utoaji wa elimu
na mafunzo nchini.”
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni