Mabadiliko ya tabia nchi
yameelezwa kuwa yamekuwa yakichangia kuangamiza mbegu nyingi za asili nchini,
kutokana na mbegu hizo kushindwa kuhimili changamoto zinazotokana na mabadiliko
hayo.
Hayo yameelezwa leo na Dk.
Emmarold Mneney kutoka Agri experience wakati akiongea kwenye mafunzo ya ufahamu wa mbegu
zilizoboreshwa kwa wahariri na waandishi wa habari wilayani Bagamoyo, mkoani
Pwani.
“Kumekuwa na dhana potofu
kuwa mbegu zilizoboreshwa zinatumika kupoteza mbegu za asili, ukweli ni kwamba
mbegu za asili zinaathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi,” alisema Dk. Mneney na
kuongeza “Mbegu nyingi za asili zinashindwa kuhimili hali ya mafuriko, mvua
chache pamoja na joto kali, hapo ndipo mbegu zilizoboreshwa zinapokuja
kusaidia”.
Dk. Mneney amesema
wanachofanya watafiki wanaozalisha mbegu zilizoboreshwa ni kurudi katika mbegu
za asili kuzizidishia nguvu ili ziweze kukabiliana na changamoto za mabadiliko
ya tabia nchi.
Akielezea historia ya tafiti
za mbegu duniani, Dk. Mneney amesema utafiti ndio uliosaidia kupatikana kwa
mbegu ya mahindi, kutoka kwenye (Mexican grass) majani ya Mexico na kuboreshwa kuwa mahindi
tunayokula leo.
“Leo tusinge kuwa tunakula
mahindi kusinge kuwa na utafiti wa mbegu, kwani mahindi yemetokana na tafiti
iliyofanywa kutoka kwa Mexican grass (Majani ya Mexico),” alisema Dk. Mneney.
Dk. Mneney amesema mbegu
zilizoboreshwa ni ufumbuzi ambao utaendelea kuwapo katika kukabiliana na
mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuboresha uzalishaji kuendana na wakati.
Pamoja na mambo mengine, Dk. Mneney amesema mafanikio ya azma ya Tanzania kuilisha dunia yatafikiwa iwapo tu Serikali itawekeza zaidi kwenye tafiti za uzalishaji wa mbegu zilizoboreshwa.
Mafunzo hayo ya siku mbili kuhusu
uzalishaji wa mbegu bora za kilimo yameandaliwa na Brains Incorporated Limited
(Media Brains) kwa kushirikiana na Alliance for a Green Revolution in Africa
(AGRA).
0 Maoni