WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje waache
malumbano na badala yake wafanye kazi kwa pamoja.
“Tumeleta fedha sh. bilioni
2 za ujenzi wa jengo la Halmashauri tangu mwaka jana lakini ninyi bado
mnabishana mjenge wapi jengo hilo. Au mnataka nizirudishe hizo fedha?” alihoji
na kujibiwa hapana.
“Tumeleta fedha mjenge jengo
jipya lakini ninyi mnataka mbomoe lililopo ili mjenge jingine wakati hapo
hakuna eneo la kutosha kupanua mji wenu. Serikali imegoma msibomoe hayo
majengo, na badala yake mnatakiwa mwende kujenga eneo la nyumba 10,” alisema.
Waziri Mkuu alitoa agizo
hilo jana (Alhamisi, Novemba 23, 2023) wakati akizungumza na watumishi, wakuu
wa idara, viongozi na wakuu wa taasisi walioko wilayani Ileje kwenye kikao cha
watumishi kilichofanyika katika ukumbi wa RM, Ileje, mkoani Songwe.
Alisema madiwani wana nguvu
zote kwenye Halmashauri lakini ni lazima pia wasikilize ushauri unaotolewa na
watalamu. Baraza la Madiwani lilikuwa linalumbana na watumishi juu ya kujenga
ofisi za Halmashauri hiyo eneo la Itumba (walipo sasa) ambalo ni dogo na
wakatoa wazo la kutaka kubomoa majengo yaliyopo ili wajenge mapya.
Maeneo yaliyokuwa
yanasababisha mvutano ni Ipapa ambalo lilipendekezwa na watumishi kwa vile ni
kubwa na litaweka majengo mengi ilhali madiwani walitaka lijengwe eneo la
Nyumba 10 kwani tayari palishajengwa ukumbi wa Halmashauri.
Waziri Mkuu aliwataka
watumishi hao wabainishe vyanzo vingine vya mapato ili kupanua wigo wa
ukusanyaji mapato wilayani humo na kwamba sh. bilioni 1.9 wanazokusanya kwa
mwaka, hazitoshelezi mahitaji. “Watumishi wa Halmashauri kila mmoja ashiriki
kubainisha vyanzo vingine vya mapato kwenye eneo lake la kazi. Na heshima ya
diwani ni kuona kata yake inachangia mapato kwenye Halmashauri yake,” alisema.
Mapema, Waziri Mkuu
alikwenda kukagua hatua iliyofikiwa kwenye ukamilishaji wa miundombinu ya
hospitali ya wilaya ya Ileje na baadaye kuzungumza na wananchi kwenye stendi ya
Itumba, wilayani humo.
Akitoa ufafanuzi wa hoja
zilizotolewa na Wabunge wa mkoa huo, Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi waliokuwa
wanamsikiliza kwamba jukumu la ujenzi wa uzio kwenye hospitali yao ya wilaya ni
la Halmashauri kwani wanapaswa kuonesha fedha ilyokusanywa imechangia kitu gani
kwenye wilaya hiyo.
“Nimeenda kukagua wodi ya
wanawake na pia wodi ya wanaume. Wodi hizi ziko umbali wa mita 10 kutoka kwenye
makazi ya watu. Tengenezeni nguzo, tafuteni wavu mpige fence ili kulinda eneo
la hospitali.
0 Maoni