WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Francis Michael na Wakuu wa Wilaya zote
za mkoa huo wahakikishe wanawasaka watu wote wanaotuhumiwa kuwapa mimba watoto
wa kike.
“Tangu Januari hadi sasa,
mkoa huu una kesi 59 za wasichana walioacha shule kwa sababu ya ujauzito lakini
ni kesi mbili tu zimeeenda mahakamani. Hizo 57 ziko wapi au zimeishia wapi? Ni
nani anazuia kesi hizi zisiende? Jeshi la Polisi, ni kwa nini hatuwafikishi
watuhumiwa kwenye vyombo vya sheria?” amehoji.
“RC na Ma-DC wote kaeni na
Kamati zenu za Ulinzi mbainishe wahusike na mhakikishe hatua kali zinachukuliwa
dhidi ya wote waliohusika,” amesema Waziri Mkuu leo (Alhamisi, Novemba 23,
2023) wakati akitoa agizo hilo mara baada ya kukagua ujenzi wa shule ya
sekondari ya wasichana Ileje.
Waziri Mkuu ambaye yuko
mkoani humo kwa ziara ya siku tatu, amesema taarifa za mkoa huo siyo kwani kesi
hizo 59 ni kwa shule za sekondari na hazijumuishi shule za msingi.
Amewakemea vijana wanaopenda
kutembea na watoto wa shule waache tabia hiyo mara moja kwani wanakatisha
maisha ya baadaye ya watoto hao. “Sheria iko wazi katika kosa hili. Adhabu yake
ni miaka 30, kijana kabla hujamfuata binti jiulize una miaka mingapi, sababu
tukikufunga utarudi ukiwa mzee,” amesema.
Akisisitiza haja ya
kuwalinda mabinti, Waziri Mkuu amesema: “Hawa ni watoto wetu, tunapaswa tuwalee
ili wakue na kuja kushika majukumu ya nchi. Rais Samia amewekeza kwao kwa kutoa
elimu bila ada. Tunapaswa tuhakikishe wanatimiza ndoto zao, kwa hiyo tuwalee
ili waweze kuhitimu,” amesisitiza.
Amewaomba masheikh na
wachungaji wakemee tabia hiyo kupitia mahubiri ya kwenye ibada.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amewapongeza wana-Ileje kwa kujenga maabara ya kompyuta kwenye
shule hiyo yenye mikondo ya kidato cha kwanza hadi cha nne ili kuhimiza
matumizi ya TEHAMA.
“Nimefurahi kuona mna jengo
maalumu la TEHAMA. Hii inaakisi malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan ya kutaka TEHAMA isambae nchi nzima.”
Amesema amefurahi pia
kusikia Halmashauri hiyo ina lengo la kuifanya shule hiyo iwe na kidato cha
tano na sita. "Mkurugenzi Mtendaji fanyeni maamuzi ili madarasa ya kidato
cha tano na sita yajengwe na muweze kuwapa fursa watoto wa kike wa wilaya hii.
Pia mtatoa chachu kwa hawa wa kidato cha kwanza hadi nne ili wasome kwa bidii,”
alisema.
0 Maoni