Serikali imeliambia Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa hali ya upatikani umeme nchini imeimarika
na sasa upungufu wa umeme umebakia kwa kiwango cha 218 MW.
Hayo yameelezwa na Naibu
Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, tarehe 9 Novemba, 2023 Jijini Dodoma
wakati akijibu maswali ya Wabunge waliotaka kufahamu mpango wa Serikali katika
kumaliza changamoto za umeme nchini.
Amesema, Serikali kupitia
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imeendelea kupunguza upungufu wa umeme
nchini kutoka MW 421 hadi MW 218 na hivyo kuimarisha Hali ya Upatikanaji wa
Umeme nchini.
Aidha, Naibu Waziri Kapinga
ameeleza zaidi kuwa, pamoja na jitihada hizo, Serikali pia imeongeza uzalishaji
wa gesi katika visima vya Mnazi Bay, Somanga na Madimba ili kuweza kuongeza
gesi ya kuzalisha umeme na kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme katika
maeneo mbalimbali nchini.
Vilevile inaendelea na
matengenezo ya mitambo ya kuzalisha umeme ili kuboresha zaidi Hali ya
Upatikanaji wa Umeme nchini.
Vile vile, ameendelea
kuwasisitiza Mameneja wa TANESCO, kuweka utaratibu mzuri wa mgao wa umeme
katika Taasisi zinazotoa huduma kwa wananchi ikiwemo Vituo vya Afya, Ofisi za
Serikali, Mashule na n.k ili wananchi waendelee kupata huduma.
Akijibu swali la msingi la
Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Christine Ishengoma aliyetaka kufahamu kumalizika
kwa tatizo la umeme katika Manispaa ya Morogoro, Mhe. Kapinga, amesema Serikali
imefunga mashineumba yenye uwezo wa MVA 120 katika Kituo cha Kupoza na
Kusambaza Umeme cha Msamvu ili kutatua changamoto ya kukatika kwa umeme kwa
mkoa huo.
Mhe. Kapinga alifafanua
kuwa, kazi hiyo ya kufunga mashineumba itagharimu kiasi cha shilingi Bilioni
10.5 na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Novemba 2023.
Kuhusu usambazaji wa umeme
katika taasisi za elimu, afya, dini, pamoja na visima, Kapinga amesema tayari
miradi inaendelea ya kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini ambapo wigo wa
usambazaji wa umeme huo umeongezwa kutoka kilomita moja hadi mbili ili Taasisi
nyingi ziweze kufikiwa.
0 Maoni