Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe amesema hakuna sababu ya
kuendelea kukiuka haki za binadamu na ukatili kwa wanawake na wasichana
kutokana na mila zenye madhara.
Mhe. Pembe ameyasema hayo wakati akihitimisha mkutano pili
wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kuhusu masuala yakutolmeza ukeketaji
uliofanyika Jijini Dar es Salaam Oktoba 9-11, 2023.
Amesema mikakati madhubuti iliyowekwa katika maazimio ya
mkutano huo yataleta mabadiliko kwa kizazi kijacho katika kupambana na ukeketaji.
"Jambo hili si tu linakiuka haki ya msingi ya wanawake
na wasichana bali pia ni ukatili mkubwa ambao sote tunakubaliana kwamba
haukubaliki," amesema Waziri Riziki.
Ameongeza kwamba teknolojia itumike kuwakutanisha wadau wote
na kubadilishana mawazo ya kutekeleza maazimio waliyojiwekea ili kutokomeza
kabisa ukeketaji Afrika na Duniani kwa ujumla.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na
Maendeleo ya Jamii Mhe. Fatma Toufiq akizungumza katika mkutano huo amempongeza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuhakikisha haki za wanawake na watoto zinalindwa kwa kukubali Programu za
kutokomeza ukeketaji zinasimamiwa.
"Hapa Tanzania juhudi mbalimbali zimefanyika tangu
mwaka 1990 hatimaye Sheria ya kupinga ukeketaji ilitungwa mwaka 1998 na katika
kuendeleza mapambano Serikali imeandaa mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza
ukeketaji pamoja sheria ya mtoto," amesema Toufiq.
Nao baadhi ya washiriki wa mkutano huo wamesema makubaliano
yaliyopatikana kwa pamoja watayafikiasha katika Mamlaka za nchi zao ili hatua
ziweze kuchukulua katika kupambana na kutokomeza vitendo vya ukeketaji Afrika
Na. WMJJWM- DSM
0 Maoni