Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa Serikali
itakuja na muafaka na utatuzi wa migogoro ya vigingi na mipasuko kati ya Wakazi
wa baadhi ya Mitaa katika Halmashauri ya Mji Geita na Mgodi wa Geita Gold Mine
Limited (GGML).
Mhe. Mavunde amesema hayo jana wakati akizungumza katika
mikutano ya hadhara yenye lengo la kusikiliza malalamiko ya wananchi wa mitaa
hiyo waliopo ndani ya vigingi vya Mgodi wa GGML.
Mitaa hiyo ni pamoja na Mgusu, Manga, Nyakabale,
Mazingamano, Samina, Ikumbayaga, Compaund, Katoma, na Nyanza.
Amesema kuwa baada ya kusikiliza hoja za pande zote za
migogoro hiyo ambazo ni kamati inayowakilisha wananchi, wananchi wenyewe,
Wamiliki wa leseni ya Uchimbaji yaani Kampuni ya GGML Serikali itakuja na
muafaka wa kumaliza tatizo hilo katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja kuanzia
sasa.
Mhe. Mavunde amesema kuwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha suala la migogoro
hiyo linatatuliwa kwa wakati ili kuwaruhusu wananchi waendelee na shughuli zao
za uzalishaji na maendeleo.
“Ndugu zangu, nimechukua maoni yenu na tunakwenda kukaa
kikao cha mwisho cha Serikali, GGML na nawaahidi hapa kwa ndani ya mwezi mmoja
kuanzia sasa nitaleta mrejesho wa msimamo wa Serikali yetu na majibu
mliyosubiria kwa muda mrefu ili kumaliza migogoro hiyo iliyodumu tangu mwaka
2000. Nina imani kama mmesubiri kwa zaidi ya miaka 23, basi hamtashindwa ndani
ya mwezi mmoja” amesema Mhe. Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa msingi wa hatua kubwa
iliyofikiwa mpaka sasa ni kazi nzuri ya mtangulizi wake, aliyekuwa Waziri wa
Madini ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto
Biteko kwa kuwa alifanyiakazi maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na
kwamba amemrahisishia kazi na kwamba Serikali inaenda kumaliza changamoto hiyo
baada ya kudumu kwa miaka kadhaa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Geita, Martine Shigella
amempongeza Waziri Mavunde kwa kutenga muda wa kuja kusikiliza malalamiko ya
wananchi hao licha ya kuwa alishakutana na Kamati inayowawakilisha na kuchukua
mapendekezo yao.
Amesema kuwa wakazi hao wamesubiri kwa muda mrefu kupata
muafaka wa changamoto zinazowakabili na kwamba hatua iliyofikia italeta faraja
kwa wakazi wa mitaa yote yenye migogoro ya vingingi na mipasuko ndani ya
Halmashauri ya Geita.
0 Maoni