Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict
Wakulyamba ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa miundombinu ya utalii
inayotekelezwa na Mradi wa REGROW ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha.
Kamishna Wakulyamba ameyasema hayo katikati ya wiki hii
alipofanya ziara ya kikazi Hifadhi ya Taifa Ruaha iliyopo mkoani Iringa, ikiwa
ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na
REGROW katika Hifadhi za Taifa Ruaha, Mikumi na katika kijiji cha Madibila
kilichopo wilayani Mbarali.
"Nimeridhishwa na kasi ya ujenzi wa miundombinu
inayoendelea kujengwa, natarajia itakapokamilika itapunguza changamoto
zilizokuwepo, pia itaongeza idadi ya watalii watakaoitembelea hifadhi hii
ambayo nimeambiwa ni ya pili kwa ukubwa Tanzania".
"Niwashukuru wenzetu wa Benki ya Dunia kwa kutupatia
msaada huu ili tuboreshe miundombinu ya utalii, uwanja huu ukikamilika utakuwa
na uwezo wa kushusha ndege za wastani zenye uwezo wa kubeba watalii 48.
Mathalani, ikishusha Ruaha, baadae Mikumi na Nyerere itawarahisishia watalii
kutembelea hifadhi nyingi zaidi kwa siku chache lakini mapato yakiongezeka
zaidi kwa taifa", aliongeza Kamishna Wakulyamba.
Sambamba na hilo pia, Kamishna wakulyamba alifanya kikao na
maafisa na askari wa Hifadhi ya Taifa Ruaha na kuwataka kuwa na nidhamu na
uadilifu katika utendaji kazi wao, alisema "msingi wa jeshi lolote ni
nidhamu cha pili kinachofanana na hicho ni uadilifu na ukiviangalia vyote
viwili ni lazima ule kiapo, hivyo ni wajibu wenu kuyaishi na kuyatenda."
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Herman
Batiho, aliahidi TANAPA kuisimamia na kuilinda miradi hiyo ili ikamilike kwa
wakati.
"Miradi hii ikikamilika kwa viwango tunavyokusudia
itaiwezesha serikali na hifadhi hii kukuza utalii Kanda ya Kusini na kuongeza
pato la Taifa kupitia shughuli za utalii na miradi mingine ya umwagiliaji
inayohudumia jamii," aliongeza Kamishna Batiho.
Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini, Steria Ndaga
alimpongeza Kamishna Wakulyamba kwa kukagua miradi na kuongea na watumishi
alisema, "kwa kipindi kifupi tangu uteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan umetembele hifadhi za Kanda ya Kusini
zote, ukikagua miradi na kuongea na watumishi, tunakuahidi maelekezo yote
uliyatoa kwetu tutayatekeleza na kuyaishi."
Miradi inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa
viwanja vya ndege viwili, nyumba kwa ajili ya malazi kwa wageni (cottages)
zenye vitanda 176 na kituo cha kutoa taarifa za utalii kwa wageni (Visitors
Information Centre).
Na. Jacob Kasiri- Ruaha.
0 Maoni