Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameutaka Mgodi wa
Singida Gold Mine unaomilikiwa na Kampuni ya Shanta Mine kuharakisha ulipaji wa
fidia kwa wananchi waliopo ndani ya eneo la leseni ambao walikuwa bado
hawajalipwa.
Mhe. Mavunde amesema hayo jana alipotembelea Mgodi huo
wilayani Ikungi mkoani Singida kujionea maendeleo ya mradi huo.
Waziri Mhe. Mavunde amesema kuwa mgodi huo umefanya kazi
kubwa ya kuhakikisha wanatimiza masharti ya leseni ya uchimbaji hivyo ni muhimu
kuharakisha ulipaji wa fidia kwa wananchi waliokuwa bado hawajalipwa.
“Niwapongeze kwa hatua mliyopiga ndani ya kipindi kifupi,
niwahimize kuharakisha suala la fidia kwa wananchi ambao bado, hii itawasaidia
nyie kufanya shughuli zenu bila malalamiko ya wananchi wa maeneo
yanayowazunguka, na kwa kuwa wamebaki wachache naamini halitachukua muda mrefu
sana," amesema Mhe. Mavunde.
Pia, Mhe. Mavunde ameuhimiza Mgodi wa Singida kuendelea
kuboresha mahusiano mazuri na wananchi wanaozunguka mgodi huo kwa kuendelea
kuwaboreshea miundombinu yao kupitia Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) pamoja
na kuwapa kipaombele wazawa katika utoaji wa huduma katika mgodini kama sheria
inavyotaka.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Singida Gold Mine, George
Kondela amesema kuwa tayari Mgodi umewalipa fidia ya ardhi wananchi 236 na
kuwajengea nyumba wananchi 12, na kwamba wanashughulikia fidia ya ardhi kwa
wananchi 53 waliosalia na nyumba za wananchi 10.
Aidha, Kobdela ameongeza kuwa mgodi huo unaendeshwa na
wazawa kwa asilimia 100 kwa hatua zote kuanzia kwenye usanifu, ujenzi na
uendeshaji.
0 Maoni