WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasili Rome, Italia ambapo
atamuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa
Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani litakalofanyika makao makuu ya Shirika
la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) kuanzia Oktoba 16, 2023 hadi
Oktoba 20, 2023.
Mkutano huo wa wakuu wa nchi na Serikali utaambatana na
maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani pamoja na maadhimisho ya miaka 78 tangu
kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).
Jukwaa hilo linatarajiwa kuwakutanisha wadau wa kilimo
wakiwemo vijana, wakulima, wazalishaji wadogo, watunga sera, wawekezaji katika
kilimo na wanasayansi duniani, wote wakiwa na lengo la kuhakikisha kunakuwa na
uhakika wa chakula ili kufikia mustakabali bora wa chakula kwa wote na bila
kumwacha mtu yoyote nyuma.
Pia, jukwaa hilo litaweka msisitizo kwa nchi husika katika
kuchukua hatua za ndani ambazo zinajikita kwenye uvumbuzi, ushirikiano,
sayansi, ushirikishwaji wa vijana, wazawa, wanawake na watu walio katika
mazingira magumu.
Katika jukwaa hilo la siku nne, Wakuu wa nchi na Serikali
kutoka nchi shiriki takribani 31 watapata fursa ya kushiriki katika Mpango wa
“Hand-in-Hand Initiative” ambapo watawasilisha mipango ya uwekezaji iliyopewa
kipaumbele nchini mwao na kuonesha fursa kwenye maeneo ambayo Mpango huo wa
Shirika la Chakula na Kilimo unasaidia Serikali kupunguza umaskini na njaa.
Viongozi Wakuu watakaohudhuria ni Rais wa Italia Mhe. Sergio
Mattarella, Rais wa Ireland Mhe. Michael Higgine, Mfalme wa Lesotho, Viongozi
wa Ujumbe kutoka Nchi Wanachama, Viongozi Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa
Mataifa (FAO, IFAD & WFP).
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni