Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Tanzania haiwezi kufikia Dira ya
Maendeleo ya 2030 huku ikiona wasichana wanaendelea kukeketwa kutokana na mila
potofu zenye madhara.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano
wa Pili wa Kimataifa wa kutokomeza Ukeketaji jijini Dar es Salaam.
Waziri Dkt. Gwajima amesema haiwezekani kujenga uwezo kamili
wa rasilimali watu kama wasichana waliowengi hawatapewa fursa ya elimu na
kufikia malengo yao kutokana na madhara ya kukeketwa.
Amebainisha kwamba, kwa mujibu wa takwimu, wanawake na
wasichana zaidi ya milioni 200 duniani wamefanyiwa ukeketaji, kati ya hao zaidi
ya milioni 20 wamefanyiwa vitendo vya ukeketaji kupitia wataalamu wa afya.
"Lazima tuseme inatosha, inatosha, inatosha. Mabadiliko
yanahitajika ili kulinda zaidi ya wanawake na wasichana milioni 68 walio katika
hatari ya kukeketwa kote duniani ambapo Afrika inachukua zaidi ya milioni 50,
ipo dhana iliyojengeka ya kuwakeketa wanawake na watoto wa kike kwa sababu za
kimila, huu ni unyanyasaji wa kijinsia ambao hauwezi kukubalika miongoni mwa
jamii,” amesema Dkt. Gwajima.
"Ukeketaji unaondoa utu wa wanawake na watoto wa kike
ikiwa ni pamoja na kuhatarisha afya zao, na maisha yao ya baadaye. Ni imani
yangu kuwa, leo katika ukumbi huu uliojaa watetezi wenye shauku, wataalam, na
watunga sera, nayaona matumaini na dhamira ya kuwa na ulimwengu ambapo kila
msichana anaweza kukua bila kivuli cha ukeketaji." Ameongeza Dkt. Gwajima.
Waziri Gwajima, amehimiza kuungana kutafuta suluhisho la
kudumu ndani ya jamii na Mataifa mengine kwa kushirikiana na viongozi wa
kimila, kidini, vikundi vya kijamii, vijana, Asasi za kiraia, viongozi wa
serikali na wadau wote, ili kuboresha maisha ya wasichana na wanawake nchini.
Dkt. Gwajima ametumia fursa hiyo kuwakumbusha vijana kuwa
wao ni chachu ya mabadiliko ya kudumu yanayotakiwa kuhusu imani na mila zenye
madhara zilizopitwa hivyo wawe kielelezo kwa jamii ya sasa.
Naye mwakilishi wa umoja wa Ulaya, Balozi Christine Grau
amesema ili kumaliza changamoto hiyo kufikia mwaka 2030 ni lazima mabinti wawe
na uhuru wa maamuzi juu ya miili yao na aidha hilo litawezekana kwa uwezeshaji
wa kiuchumi na kielimu.
“Mabadiliko hayakwepeki na mila hubadilika kila baada ya
muda hivyo jamii zetu hazina budi kuachana na mila kandamizi ikiwemo ukeketeji
kwa mabinti kwani mila hii ni unyanyasaji wa kijinsia na ina madhara makubwa
kwa wanawake,” amesema Balozi Grau.
Janeth Sallah Njie ni Kamishna anaeshughulika na kutetea
haki za wanawake kutoka ACHPR, amesema, bado kuna changamoto ya baadhi ya jamii
kwenda nchi za jirani kuwafanyia ukeketaji mabinti na mfano mzuri ni nchi za
Kanda ya Afrika mashariki (Ethiopia, Somalia, Uganda na Tanzania) kwenda nchini
Kenya.
Halikadhalika, Mwakilishi mkazi wa Unicef, Elke Wische
amesema kuna ulazima wa kuimarisha sera zinazomlinda mtoto wa kike katika nchi
zenye changamoto hii ya ukeketaji.
Mkutano huo wa siku mbili wenye kaulimbiu isemayo
"Mabadiliko katika Kizazi" una lengo la kutoka na maazimio na hatua
stahiki kuhusu kutokomeza ukeketaji ifikapo mwaka 2030.
Na WMJJWM- DSM

0 Maoni