Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.
Hussein Ali Mwinyi ametoa rai kwa mashirika ya utangazaji ya umma kuwekeza na
kuwa na vitendea kazi vya kisasa vinavyoendana na mabadiliko ya sayansi na
teknolojia duniani katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali kwa maendeleo
endelevu.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 10 Oktoba 2023
wakati alipofungua mkutano mkuu wa 30 wa mashirika ya utangazaji ya umma kutoka
nchi za Kusini mwa Afrika (SABA) uliofanyika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Airport,
Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha Rais Dk. Mwinyi ameeleza kuwa ni wakati sahihi
kuhakikisha vyombo vya utangazaji vya umma vinakuwa na vyanzo vya uhakika vya
mapato vihimili changamoto za kifedha kwa kutimiza ipasavyo dhana ya kukuza, kulinda
na kutangaza utamaduni wa mwafrika.
Halikadhalika Rais Dk. Mwinyi amewakaribisha wajumbe wa
mkutano huo kutembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana Zanzibar ikiwemo
urithi wa dunia wa Mji Mkongwe pia na vivutio vya upande wa Tanzania bara
ikiwemo Mlima wa Kilimanjaro, Hifadhi za Taifa za Serengeti, Ngorongoro na
Manyara.
Mkutano huo wa siku tatu utajadiliana kwa kina nafasi ya
TEHAMA na mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali Afrika ili kuleta
maendeleo endelevu.
0 Maoni