WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na
wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yanayofadhili miradi ya mazingira na
mabadiliko ya tabianchi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jana katika Ofisi ndogo
za Ofisi Makamu wa Rais Jijini Dar es Salaam, Waziri Jafo alipokea taarifa
kutoka kwa wawakilishi hao kuhusu uwasilishaji wa andiko la taarifa la
vipaumbele miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi itakayowasilishwa
katika Baraza la Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) mwishoni mwa mwezi huu.
Waziri Jafo amesema kikao hicho na wawakilishi wa mashirika
hayo sehemu ya ufuatiliaji wa maadhimio ya Mkutano Mkuu wa Saba wa Mfuko wa
Mazingira wa Dunia – GEF, uliofanyika katika Mji wa Vancouver nchini Canada
ambapo ambapo nchi zilizoendelea na zinazoendelea zilikubaliana kuwezesha
ukusanyaji wa fedha katika shughuli za uhifadhi wa mazingira duniani.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo amesema Tanzania bado ina mahitaji
makubwa ya rasilimali fedha kutoka GEF kwa ajili ya kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabianchi, hivyo mara baada ya kumalizika kwa kwa mkutano huo
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais iliunda timu ya wataalamu kwa ajili ya
kupitia vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kwa
ajili ya uratibu wa maombi ya fedha za utekelezaji na usimamizi wa miradi hiyo.
“Tanzania ni mhanga mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi. Leo
ukitazama Wilaya ya Simanjiro utaona ni kwa jinsi gani wafugaji wanavyohangaika
na mifugo yao, si hapo tu na Mpwapwa napo hali nayo si nzuri…hivyo tunahitaji
miradi mingi zaidi ya ufadhili wa fedha ili kuzinusuru jamii zetu,” amesema
Waziri Jafo.
Kwa upande wake Mshauri wa Rais, masuala ya Mabadiliko ya
Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi ameyashukuru mashirika hayo kwa
kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya mazingira hapa nchini na kuongeza kuwa
mahitaji makubwa zaidi ya fedha bado yanahitaji ili kuleta manufaa kwa jamii na
taifa kwa ujumla.
Akitolea mfano Dkt. Muyungi amesema Serikali imeendelea
kutekeleza miradi mbalimbali mradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya
tabianchi ikiwemo ujenzi wa mradi wa kingo za bahari ya Hindi katika maeneo ya
barabara ya Barack Obama (Ocean Road) ambao umelenga kuzuia mmomonyoko wa
udongo baharini.
Dkt. Muyungi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na
wadau mbalimbali yakiwemo mashirika ya kimataifa ili juhudi za pamoja ziendelee
kuimarishwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na
kuhakikisha miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira inaendelea kuibuliwa
katika jamii.
Kwa upande wao wawakilishi wa mashirika hayo wameihakikishia
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuwa maandalizi muhimu ya uwasilishaji
wa taarifa za vipaumbele vya miradi ya mazingira inayosimamiwa na GEF
imekamilika na kwa pamoja wameishukuru Serikali kwa juhudi kubwa inazoendelea
kufanya katika kushirikiana na wadau.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Mazingira la Umoja
wa Mataifa (UNEP) Bi. Clara Makenya amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana
na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha juhudi za pamoja zinaendelea
kuchukuliwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo
ufadhili wa miradi na uwezeshaji wa fedha.
“Katika andiko letu UNEP tutakalowasilisha GEF tumeainisha
maeneo mapya ya miradi kwa Tanzania…Tayari tuna miradi katika maeneo
matano…Tumepanga kuangalia awamu ijayo tuanze kuitekeleza Zanzibar na maeneo ya
Mikoa ya Nyanda za Juu kusini” amesema Bi. Makenya.
Mashirika yahudhuria kikao hicho kilichoitishwa Mhe. Waziri
Jafo ni Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Mazingira
la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Shirika la Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO)
ambapo mashirika hayo yanafadhili miradi inayotekelezwa katika maeneo
mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Miradi inayofadhiliwa na mashirika hayo ni pamoja na Mradi
wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia (EBARR) na
Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS).
0 Maoni