Watu watano washikiliwa kwa kutorosha madini ya dhahabu

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na kikosi kazi cha tume ya madini, linawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za kutorosha madini na kufanya biashara ya madini bila kuwa na kibali.

Kamanda wa Polisi Mbeya ACP Benjamin Kuzaga amesema watuhumiwa waliokamatwa ni, Masunga Kidishi (43), Timoth Simbu (26), Ngunje Ideshi (41), Ester John (25) na Baraka Silwani (28) wote wafanyabiashara na wakazi wa Chokaa Wilaya ya Chunya.

Watuhumiwa walikamatwa Oktoba 26, 2023 huko Mtaa wa kibaoni wilayani Chunya wakiwa na madini aina ya dhahabu vipande 160 vyenye uzito wa gramu 6,933.6 wakiwa hawana nyaraka "transport permit” wakiwa wanatorosha madini hayo kwenda kuuza nje ya mfumo wa soko la dhahabu.

Wataalamu kutoka Wizara ya Madini wanaendelea na uchunguzi ili kujua thamani halisi ya madini hayo, amesema Kamanda Kuzaga.

Aidha, dhahabu vipande 145 vilipatikana baada ya kupekua kwenye makazi ya mtuhumiwa Ngunje Ideshi.

Kamanda Kuzaga amesema awali kabla ya kukamatwa vipande hivyo vilikamatwa vipande 15 vya dhahabu kwenye Gari T.796 DTT IST iliyokuwa na watuhumiwa Timoth Simbu na Ngunje Kidishi.

Watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa na mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Chapisha Maoni

0 Maoni