SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekabidhi rasmi mashamba ya Wanyamapori ya Lente, Loldebes na Amani
yaliyopo wilaya ya Monduli Mkoani Arusha kutoka kwa Msajili wa Hazina na kwenda
kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa ajili ya shughuli
za uhifadhi na uendelezaji wa utalii.
Mkuu wa wilaya ya Monduli Mhe. Joshua Nassari ambaye alikuwa
mgeni rasmi katika hafla ya makabidhiano ya mashamba hayo iliyofanyika ndani ya
eneo la mashamba almaarufu "Makuyuni Wildlife Park" amemshukuru Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi
yake ya kubadilisha matumizi ya mashamba kutoka kwenye shughuli za kilimo na
kurasimisha ili yaweze kutumika kwa shughuli za uhifadhi na uendelezaji wa
utalii.
Mhe. Nassari amesema maamuzi hayo yanakwenda kufungua fursa
nyingi zenye tija kwa wakazi wa Monduli kutokana na uwekezaji utakaofanywa na
TAWA katika eneo hilo na kuitaka TAWA iliendeleze eneo hilo kwa haraka kwakuwa
ni eneo muhimu, lenye rasilimali nyingi na linafikika kirahisi.
Mkuu huyo wa Wilaya ameipongeza TAWA kwa juhudi inazozifanya
katika kuboresha utendaji wa Taasisi.
"Niwapongeze sana TAWA kwa "efforts" (juhudi)
ambazo mmezifanya tumeona mageuzi makubwa mno kwenye Taasisi yenu kwa miaka ya
hivi karibuni, tunaamini kwamba Ile "pace" mnayokwenda nayo na huku
kwetu tunaamini kufikia mwakani mapato yetu ya Halmashauri yatakuwa
yanaongezeka" amesema.
Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Mej. Jen. (Mstaafu)
Hamis Semfuko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri
Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa kuridhia TAWA ikabidhiwe mashamba
hayo kwa ajili ya Uhifadhi na uendelezaji wa utalii
Aidha, Semfuko amesema kwakuwa eneo hilo lina fursa kubwa ya
Utalii TAWA imelipa jina la kibiashara la "Makuyuni Wildlife Park" na
kwamba maono ya Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA ni kuongeza mapato na kuimarisha
Uhifadhi na italitumia eneo hilo kwa utalii wa picha na kwa kuanza itajenga
miundombinu wezeshi ili kuwezesha shughuli za uhifadhi na Utalii kufanyika
kikamilifu pamoja na kuvutia wawekezaji
Kwa Upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi
Nyanda kutokana na Imani kubwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
TAWA hata kuikabidhi mashamba hayo, TAWA italipa Imani hiyo kwa kuwa wabunifu
katika kuongeza mapato katika eneo hilo, ikizingatiwa kuwa eneo hilo awali
lilitumika kama mashamba ya kilimo lakini kutokana na umuhimu wake kiuhifadhi
Serikali imeamua litumike kwa shughuli za kiuhifadhi.
Pia, amewaomba wananchi wanaozunguka eneo hilo kuendelea
kushirikiana na TAWA katika ulinzi wa rasilimali zilizopo na kuhakikisha
zinanufaisha jamii kupitia shughuli za Utalii
Awali akielezea historia ya mashamba hayo, Mkurugenzi wa
ubinafsishaji, ufuatiliaji na tathmini - Ofisi ya Msajili wa Hazina Mohamed
Nyasama amesema mnamo tarehe 02 Juni, 2022 Msajili wa Hazina kupitia barua yake
alikabidhi mashamba hayo kwa TAWA kwa ajili ya Usimamizi wa muda wakati
wakisubiri maelekezo ya Mamlaka.
Ameongeza kuwa tarehe 27 februari 2023 Mamlaka ilitoa
maamuzi na kupitia barua ambayo iliandikwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya fedha
ilitoa maelekezo kuhusiana na matumizi ya eneo hilo na kupitia barua ya Katibu
Mkuu kiongozi walitaarifiwa kuwa Mamlaka imeridhia mapendekezo ya kamati kuwa
mashamba ya steyn (yaan shamba la Lente, Loldebes na Amani) yakabidhiwe rasmi
kwa TAWA ili yatumike kwa ajili ya uhifadhi na uendelezaji wa utalii
Na Beatus Maganja, Arusha
0 Maoni