Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki amesema
kuwa maandalizi ya Onesho la saba la Utalii la Kimataifa la Swahili
International Tourism Expo –S!TE 2023 yamekamilika ambapo kwa mara ya kwanza kutakuwa na bustani ya
wanyama hai
Akizungumza kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari jana katika
Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam amesema onesho hilo
litafanyika kuanzia Oktoba 6 - 8 mwaka huu ambapo wageni na wadau muhimu wa
sekta kutoka maeneo mbalimbali duniani watahudhuria.
“Katika kipindi chote onesho hili limekuwa jukwaa muhimu na
lenye ushawishi kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi walio katika mnyororo
wa huduma za utalii.” Amefafanua Mhe. Kairuki.
Waziri Kairuki amewataja baadhi ya wadau watakaoshiriki
kwenye maonesho ya mwaka huu kuwa ni pamoja na Mabalozi wa nchi mbalimbali,
Bodi za Utalii kutoka nchi za Afrika zikiwemo Uganda na Malawi, Waoneshaji
(Exhibitors) zaidi ya 100 kutoka ndani na nje ya nchi. Wanunuzi wa biashara za
utalii (Buyers) zaidi ya 70 kutoka katika masoko yetu ya Kimkakati ya kimataifa
hususan, Ulaya, Amerika na Asia.
Aidha, amesema onesho la mwaka huu litapambwa na Bustani ya
Wanyamapori hai ili kuwavutia watembeleaji (visitors) na kuhamasisha Utalii wa
ndani, pamoja na Jukwaa la Uwekezaji la Utalii (Tanzania Tourism Investment
Forum-TTIF) na ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kuja kutembelea na kuona
hazina na urithi wa utalii wa Tanzania pia
“Natoa rai kwa watanzania, wawekezaji, na wadau wengine wa
utalii kushiriki kikamilifu onesho la SITE 2023, ambalo ni fursa ya muhimu
kukutana na wadau wenzenu waliopo katika mnyororo wa thamani wa Sekta ya
Utalii, ili kwa pamoja tuhakikishe sekta hii inapiga hatua tukitambua melengo
makubwa tuliyonayo ya kufikia watalii milioni 5 na mapato ya Dola za Marekani
Bilioni 6 ifikapo mwaka 2025. Halikadhalika kuendelea kuitangaza nchi yetu kimataifa
kupitia utambulisho wetu wa Tanzania, Unforgettable na Programu ya Tanzania –
The Royal Tour.” Amesisitiza Mhe. Kairuki.
Waziri Kairuki ametoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea
mtandao wa site.tanzaniatourism.go.tz ili kuona mambo muhimu yanayohusu onesho
hili ikiwa ni pamoja na semina mbalimbali, midahalo inayoangazia mada za utalii
na fursa za uwekezaji ambapo amesema Kauli mbiu ya Onesho la S!TE 2023 ni:
Utalii Unaowajibika kwa Maendeleo Jumuishi.
0 Maoni