Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inaandaa
mkakati mpya wa ukusanyaji mapato utakaolenga kuongeza mapato ya Taasisi hiyo
mara dufu ya makisio yake ya Mwaka wa fedha 2023/2024.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula
Misungwi Nyanda katika kikao kazi na wakuu wa Kanda na wakuu wa mapori wa TAWA
chenye lengo la kuboresha utendaji kazi katika nyanja za kuongeza mapato na
Uhifadhi kwa ujumla, kilichofanyika ukumbi wa NCAA Jijini Arusha
Kamishna Mabula amesema suala la kuongeza Kasi ya ukusanyaji
mapato ni maelekezo mahsusi kutoka kwa Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii
Mhe. Angellah Kairuki na hivyo utekelezaji wake unapaswa kuanza haraka
iwezekanavyo
"Hili suala la ukusanyaji mapato lisisubiri huo mkakati
unaoandaliwa lianze Kuanzia Sasa hivi, Kila kitu unachokiona kwenye eneo lako
ni rasilimali hakikisha unakitumia kuingiza mapato," amesisitiza Kamishna
Mabula.
Kamishna Mabula pia ametoa msisitizo katika suala zima la
udhibiti wa Wanyamapori wakali na waharibifu na kuwataka maofisa hao kutafuta
mbinu mbadala za kuhakikisha Wanyamapori hao hawaendelei kuleta madhara kwa
maisha na mali za binadamu.
Aidha, amewataka maofisa hao kuzingatia maelekezo aliyoyatoa
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili Kamishna Benedict Wakulyamba wakati wa
semina elekezi kuhusiana na Wanyama Wakali na Waharibifu.
Kwa Upande wake Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mlage
Kabange amesema mtaji namba moja wa TAWA ni ulinzi wa maeneo yote waliyopewa
kuyasimamia kwani maeneo yanapokuwa salama ndipo uzalishaji mapato unaongezeka
ikizingatiwa kuwa asilimia 70 ya mapato ya TAWA yanatokana na shughuli za
Uwindaji wa Kitalii.
Sanjari na hilo, amesisitiza kuongeza Kasi ya utekelezaji wa
zoezi la kuweka alama za mipaka katika maeneo yote yaliyo chini ya Usimamizi wa
Taasisi huku wakifuata miongozo na maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali
Na. Beatus Maganja- Arusha
0 Maoni