WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan ana utashi mkubwa wa kisiasa katika kukuza sekta ya michezo kwa kufanya
uwekezaji na mabadiliko kwenye sekta hiyo.
Amesema hayo leo (Jumatano, Oktoba 4, 2023) wakati wa hafla
ya kukabidhi shilingi milioni 500 kwa timu ya Taifa ya mpira wa miguu (Taifa
Stars) ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Dkt. Samia kwa timu hiyo baada ya
kufuzu michuano ya AFCON 2024.
“Uamuzi wa Rais Dkt. Samia wa kuridhia asilimia tano ya kodi
itokanayo na michezo ya kubashiri (sports betting) ipelekwe katika Mfuko wa
Maendeleo ya Michezo ili kusaidia shughuli za maendeleo ya michezo hapa nchini
umelenga kuikuza zaidi sekta hiyo.”
Ameongeza kuwa hatua ya Rais Samia kuiundia sekta ya michezo
wizara yake ni uthibitisho tosha kwamba anataka kuhakikisha kwamba Tanzania
inafikia hatua ambazo mataifa mengine yameshafikia kwenye sekta ya michezo.
“Hayo ni baadhi tu ya mambo ya kujivunia katika kipindi hiki
cha utawala wa Jemedari na nguli wa michezo, kiongozi shupavu, mama yetu
mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.”
Kabla ya kukabidhi hundi hiyo, Waziri Mkuu alikagua
ukarabati unaoendelea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwemo vyumba vya
wachezaji kubadilishia nguo, chumba cha matibabu, hali ya uwanja, chumba cha
VAR na chumba cha kufuatilia kamera za ulinzi wa uwanjani. Alisema ameridhishwa
na kazi ya ukarabati inayoendelea kwenye awamu hiyo ya kwanza.
Akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro alisema kutokana na ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan, vijana wa timu ya Taifa walipambana hadi wakafuzu kwenda
AFCON kwa mara ya tatu.
Alisema Tanzania, Kenya na Uganda ziliungana na kuomba kuwa
wenyeji wa mashindano ya AFCON kwa mwaka 2027. “Nchi hizi tatu, kwa mara ya
kwanza zitakutana huko Mombasa mwezi huu wa kumi ili kuratibu shughuli hii kwa
pamoja,” alisema.
Mapema, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF),
Wallace Karia alisema mbali na kujenga viwanja vipya huko Arusha na Dodoma,
Benjamin Mkapa na Amri Abeid ni miongoni mwa viwanja vinavyofanyiwa ukarabati
ili vitumike kufanya mazoezi wakati wa mashindano ya AFCON.
Aliiomba Serikali iwasaidie kupata usafiri wa moja kwa moja
kwenda Morocco ili wawahi kurudi nyumbani kwa ajili ya mechi ya marudiano.
0 Maoni