Alex Lameck (18) Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Tamabu na
Mkazi wa Mission wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza amepandishwa kizimbani
katika mahakama ya wilaya ya Sengerema na kusomewa shtaka la kujeruhi.
Mwanafunzi huyo amesomewa shtaka hilo leo Oktoba 4,2023,
katika kesi ya jinai namba 114/2023, ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo kinyume
na kifungu namba 225 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 toleo la mwaka
2022.
Akisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Evod
Kisoka, Wakili wa Serikali Morice Mtoi, amesema mshtakiwa alitenda kosa hilo
tarehe 25.09.2023 katika shule ya Sekondari Tamabu wilayani humo kwa kumjeruhi
kwa panga kichwani Stanford Mgaya (37) ambaye ni mwalimu katika shule hiyo.
Mshtakiwa amekana shtaka hilo na amedhaminiwa baada ya
kutimiza vigezo vya dhamana na shauri hilo limeahirishwa hadi tarehe 11.10.2023
kwa ajili ya kusoma hoja za awali.
0 Maoni