Jumla ya vijana 6,000 kutoka Shirika la Suma JKT la Jeshi la
Wananchi Tanzania, (JWTZ) wameanza kuwasili wilayani Handeni mkoani Tanga
kwa ajili ya shughuli ya ujenzi wa nyumba 5,000 katika kijiji cha Msomera.
Akizungumzia kuhusu ujio wa vijana hao, wilayani Handeni, Mkuu
wa Jeshi la Kujenga Taifa, (JKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema shughuli
yao itakuwa ni ujenzi wa nyumba hizo na tayari vijana 500 wamesharipoti kwenye
mradi na wengine wanaendelea kuingia.
Amesema tayari wameshapokea fedha kutoka uongozi wa Mamlaka
ya Hifadhi Ngorongoro, kwa ajili ya kujenga nyumba hizo ambapo muda wa ujenzi
utakuwa ni miezi sita kuanzia Oktoba 2023 hadi Machi 2024.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Hifadhi
Ngorongoro Jenerali Venance Mabeyo kwa upande wake amezitaka wizara za kisekta,
kuharakisha ujenzi wa miundombinu katika eneo la mradi kijiji cha Msomera ili
wahusika waweze kuanza kazi.
Mkuu wa wilaya ya Handeni Albert Msando amesema wanatarajia
kusimamia ujenzi huo kwa wakati, ili kuepukana na mabadiliko ya hali ya hewa
hasa mvua ambayo inaweza kuleta changamoto katika kusafirisha vifaa vya ujenzi.
Jumla ya Shilingi bilioni 97 zinatarajiwa kutumika katika
ujenzi wa nyumba hizo 5000, kwa ajili ya wananchi watakaohama kwa hiari kutoka
eneo la Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro.
0 Maoni