Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema kampeni
ya upandaji wa malisho ya mifugo na uchimbaji wa visima na malambo katika
mashamba ya wakulima binafsi inalenga kutatua migogoro ya ardhi nchini.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti amesema
hayo wilayani Mvomero mkoani Morogoro wakati akihitimisha jukwaa la maandalizi
ya kampeni hiyo ijulikanayo kama "Tutunzane Mvomero" na kusema
migogoro mingi ya ardhi imekuwa ikitokana na kutokuwa na mpango wa matumizi
bora ya ardhi katika vijiji na kwenye maeneo ambayo tayari mipango hiyo
usimamizi wake unakuwa hafifu.
Kampeni hii ina kauli mbiu isemayo “Mfugaji mtunze mkulima
na mkulima mtunze mfugaji ili kulinda mazingira yetu” inalenga kuwaelimisha
kwanza kuanza kumiliki ardhi kwa ajili ya kuoata malisho ya mufugo yao na
kuanza kufuga mifugo inayoendana na eneo la ardhi wanayomiliki ili kuondokana
na migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kutokana na
wafugaji kuhamahama.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi
amewahimiza wafugaji kuendelea kumiliki maeneo kwa ajili ya ufugaji na kufuata
sheria na taratibu zilizopo ili wasiingie kwenye migogoro ambayo inaweza
kusababisha uvunjifu wa amani.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejipanga kuhakikisha haki
inatendeka kwa kila mwananchi hivyo ikiwa kosa linakuwa kwa mfugaji au mkulima
basi kila mmoja atachukuliwa hatua kulingana na sheria na taratibu zilizopo.
0 Maoni