Waziri wa Ardhi Nyumba na Maedeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa
ametoa siku saba kupatikana suluhu ya changamoto za urasimishaji makazi holela
wa makazi katika mkoa wa Dar es Salaam.
Agizo la Waziri Silaa linafuatia mkoa wa Dar es Salaam kuwa
moja ya mikoa yenye malalamiko mengi ya urasimishaji makazi holela zoezi ambalo
lilianza mwaka 2013 na kutarajiwa kukamilika mwaka huu 2023.
Silaa ametoa agizo hilo jana alipokutana na uongozi wa mkoa
wa Dar es Salaam na watendaji wa sekta ya ardhi kujadili utekelezaji wa ilani
ya Chama cha Mapinduzi kwa upande wa sekta ya ardhi.
"Kero ni kubwa nikitoka hapa naenda kukaa na wenzangu wizarani
ili zoezi hili katika mkoa wa Dar es Salaam lifanyike haraka na lifike mwisho,"
alisema Mhe. Silaa.
Amesema, pamoja na hatua iliyofikiwa kwenye urasimishaji,
utekelezaji wa programu hiyo umekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo makampuni
yaliyopewa kazi hiyo kushindwa kukamilisha kwa wakati huku wananchi wakikosa
imani kwa makampuni na kuacha kuhangia gharama za utekelezaji kazi hiyo na
kusababisha zoezi hilo kukwama katika maeneo mengi.
Waziri Silaa ameeleza kuwa, kama kuna makampuni yamefanya vibaya
katika zoezi la urasimishaji basi yapewe adhabu zake na wananchi wajue na iwapo
kuna makampunii kazi zo zimekwama basi zikwamuliwe na kama kuna wananchi
waliokwama kupata hati basi wapatiwe.
Amesema, athari za zoezi hilo la urasimishaji kwa mkoa wa
Dar es Salaam ni kubwa sana ukilinganishwa na mikoa mingine huku akibainisha
kuwa jumla ya vipande vya ardhi vilivyotambuliwa ni 625,639 kati ya hivyo
upangaji umekamilika kwa viwanja 556,755 ilihali upimaji ukiwa umefanyika kwa
viwanja 125,035 na umilikishaji ukiwa viwanja 28,902 pekee.
Kwa mujibu wa Waziri Silaa, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
amemteua na kumuamini afanye kazi ya ardhi na yeye ameamua kufanya hivyo ili
kupunguza kama siyo kuondoa kabisa kero za ardhi nchini.
"Mimi naamini kwa kero za dar es salaam na umuhimu wa
mkoa huu tuache mengine yote na tutafute suluhu ya urasimishaji kwa mkoa wa Dar
es Salaam," alisema Waziri Silaa.
Vile vile, Waziri Silaa ameongeza kuwa, katika kuhakikisha
wizara yake inaondoa kero za ardhi nchini wamejipanga kuchukua hatua mbalimbali
ikiwemo kusogeza huduma karibu na wananchi.
Ametaja baadhi ya hatua za usogezaji huduma kwa wananchi
kuwa, ni kuwa na ofisi za ardhi kwa kila mkoa zikioongozwa na makamishna wa
ardhi wasaidizi wa mikoa tofauti na huko nyuma ambapo huduma zilikuwa
zikitolewa kwenye ofisi za kanda.
Aidha, amesema kwa ile mikoa yenye changamoto kubwa kama Dar
es Salaam wameweka makamishna wa ardhi wasaidizi wa mikoa wawili lengo likiwa
kurahisisha utendaji kazi.
Hata hivyo, amesema wizara yake inafikiria kuwa na mpango wa
ikiwezekana kuwa na mikoa maalum ya ardhi katika wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam.
Na. Munir Shemweta- WANMM
0 Maoni