RC Chalamila apokea msaada wa vifaa tiba kutoka DKT International

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amepokea vifaa tiba vya msaada uliotolewa na Shirika la DKT international ambavyo ameelekeza vipelekwe katika Wilaya ya Kigamboni na Ubungo za Jijini Dar es Salaam.

Akipokea msaada huo wa vifaa tiba RC Chalamila amelishukuru shirika hilo kwa kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya Afya hapa nchini, mchango uliotolewa ni wa thamani kubwa, ametoa rai kwa wadau wengine wa afya katika mkoa kuiga mfano na kuunga mkono juhudi za Serikali katika katika mkoa.

"Rais Dkt Samia Suluhu amekuwa akitoa pesa nyingi na anaendelea kutoa katika kuboresha sekta ya afya, ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na hospitali zimeendelea kujengwa kila kona hivyo kuunga mkono juhudi hizi ni kumpa nguvu Rais aendelee kupambana zaidi kwa masilahi mapana ya Watanzania," alisema RC Chalamila.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam amewataka wahusika wa Wilaya ya Ubungo na Kigamboni kuhakikisha wanavitunza vifaa tiba walivyopatiwa ili viweze kutumika kwa muda mrefu kwa manufaa ya umma.

Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt Rashid Mfaume ameanisha vifaa tiba vilivyotolewa na Shirika la DKT International ikiwemo vitanda kwa ajili ya operesheni, makabati na viti mwendo, pia amewaomba kuendeleza ushirikiano na mkoa katika kutekeleza afua mbalimbali za kukabiliana na magonjwa ya ngono, uzazi wa mpango na Ukimwi.

DKT International ni shirika lisilo la Kiserikali ambalo linajishughulisha zaidi na upangaji uzazi, kuzuia VVU/UKIMWI na uzuiaji mimba kwa njia salama.


Chapisha Maoni

0 Maoni