UWEPO wa chakula cha kutosha ni muhimu kwa maendeleo ya
Taifa lolote kwa kuwa bila ya kuwa na uhakika wa chakula hata usalama wa nchi
nao huyumba, hivyo ni vyema kujiwekea mikakati ya kuzalisha chakula cha kutosha.
Katika kudhihirisha
umuhimu wa usalama wa chakula nchini, hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia
Suluhu Hassan katika mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani
lililofanyika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo
(FAO) kuanzia Oktoba 16, 2023 hadi Oktoba 20, 2023.
Mkutano huo wa wakuu wa nchi na Serikali ulimbatana na
maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani pamoja na maadhimisho ya miaka 78 tangu
kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).
Jukwaa hilo ambalo liliwakutanisha wadau wa kilimo wakiwemo
vijana, wakulima, wazalishaji wadogo, watunga sera, wawekezaji katika kilimo na
wanasayansi duniani, wote wakiwa na lengo la kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa
chakula ili kufikia mustakabali bora wa chakula kwa wote.
Akizungumza katika jukwaa hilo Mheshimiwa Majaliwa amesema
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar zimeweka mipango inayolenga kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa
wa chakula kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi na ziada kuuza nje ifikapo
2030.
Mheshimiwa Majaliwa amesema katika kuhakikisha mipango hiyo
inafanikiwa, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo
ujenzi wa reli ya kisasa, barabara na nishati vijijini ili kurahisisha shughuli
za kilimo. “Maboresho mengine ni ujenzi wa viwanda vya kuzalisha pembejeo za
kilimo na kuhamasisha wakulima kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji.”
Waziri Mkuu alisema licha ya jitihada za kuboresha sekta ya
kilimo ambazo zimewekwa ndani za kushirikisha vijana na wanawake kuhakikisha
kwamba wanaongeza teknolojia, kutumia mbolea kwenye kilimo, pamoja na
ushirikishaji wa sekta binafsi, pia Serikali ameamua kuungana na FAO kupitia
Mkurugenzi Mkuu na ameahidi kuiunga mkono mipango hiyo.
Mheshimiwa Majaliwa alisema katika kuhakikisha Taifa
linafanikiwa kwenye utekelezaji wa mpango wake wa kuwa mzalishaji mkubwa wa
chakula, Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan imeanza kupanua wigo wa kilimo kutoka cha kutegemea mvua na kujikita
zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji, ambapo imetenga shilingi bilioni 900.
Waziri Mkuu alisema kuwa mbali na maboresho hayo
yaliyofanyika katika sekta ya kilimo, pia Serikali inawasimia wakulima kuanzia
hatua za awali za maandalizi ya mashamba, upandaji wa mazao, uvunaji na
uhifadhi wa mazao hayo hadi kwenye utafutaji wa masoko kupitia maafisa ugani
ambao wapo hadi vijijini.
Alisema Serikali imeanza kusajili wakulima katika mfumo wa
kidigitali lengo likiwa ni kujua idadi ya wakulima, ukubwa wa mashamba na aina
ya mazao wanayolima ili kurahisisha ufikishwaji wa huduma za ugani. “Kilimo
ndio maisha, kilimo ndio chakula, tunataka kujikita zaidi katika kilimo cha
umwagiliaji kwa kutumia mabwawa yetu. Tunataka tujiridhishe kuwa hakuna
Mtanzania atayekufa kwa kukosa chakula.”
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa
Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Dkt. Qu Dongyu alisema Tanzania ina fursa
kubwa ya kuendeleza sekta ya kilimo na uchumi wa buluu, hivyo Shirika lao liko
tayari kushirikiana na Tanzania katika kutoa msaada wa kitaalam pamoja na
kukuza mifumo ya uzalishaji wa chakula.
Aidha, Dkt. Qu Dongyu alisema kuwa Shirika hilo limevutiwa
na mradi wa kuwawezesha vijana unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania wa Jenga
Kesho Iliyobora “Building Better Tomorrow” (BBT). “FAO tutaunga mkono mradi huu
ili Serikali ya Tanzania iweze kutimiza malengo ya kuwainua vijana na wanawake
kwenye sekta ya kilimo kama ilivyo moja ya agenda kwenye mkutano wa FAO wa
mwaka 2023”.
Mkurugenzi huyo wa FAO amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza sekta ya kilimo pamoja na kuboresha
mahusiano na mashirika ya kimataifa, ambapo ameahidi kutembelea Tanzania mwaka
2024 kwa ajili ya kujionea maendeleo katika sekta ya kilimo pamoja na kupanua
wigo wa majadiliano kati ya Tanzania na Shirika hilo ili kuendelea kuwezesha
zaidi sekta ya kilimo na uchumi wa Buluu.
Naye, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamata Shaame Hamisi alisema kwa sasa
Serikali inafanya maboresho makubwa katika sekta ya kilimo na miongoni mwa
maboresho hayo ni utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji ambayo inalenga
kuimarisha upatikanaji wa chakula.
Awali, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema
Serikali imeendelea kuwashawishi vijana kushiriki katika shughuli za kilimo
kwani mbali na kuongeza uzalishaji wa chakula, pia kilimo ni miongoni mwa sekta
zinazotoa ajira nyingi, hivyo watakuwa wamejihakikishia ajira.
Licha ya kuhudhiria alimuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani na
maadhimisho ya miaka 78 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la
Chakula na Kilimo (FAO), pia Waziri Mkuu alifungua katika Jukwaa la Tatu la
Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia lililofanyika Palazzo Regione
Lombardia, Milan nchini Italia pamoja na kutembelea shamba la kisasa la ufugaji
wa ng'ombe.
JUKWAA LA BIASHATA TANZANIA NA ITALIA
Oktoba 19, 2023 Waziri Mkuu alifungua kongamano la tatu la
Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia, ambapo
Mheshimiwa Majaliwa alitoa wito kwa Watanzania walioshiriki katika jukwaa hilo
wahakikishe wanatumia vizuri fursa walizozipata kutoka kwenye jukwaa hilo,
ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano kwa wawekezaji na wafanyabiashara
walioonesha nia ya kuja kuwekeza nchini.
Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali ya awamu ya sita
inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeondoa tozo na urasimu
uliokuwepo awali kwa lengo la kurahisisha shughuli za biashara na uwekezaji
nchini, hivyo alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji
wa Italia waje kuwekeza nchini.
“Msisitizo wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na
mkakati wa Serikali ni kuwahamasisha wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa
mbalimbali nchini waje kuwekeza katika ujenzi na kuzalisha bidhaa hizo nchini
ili zipatikane kwa wingi na kwa urahisi.”
Mheshimiwa Majaliwa alisema kupitia jukwaa hilo
wafanyabiashara na wawekezaji wengi kutoka nchini Italia wameonesha nia ya kuja
Tanzania kwa ajili ya kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo, madini,
uvuvi, afya, mifugo, viwanda na utalii, hivyo amewataka viongozi na watendaji
wa wizara zinazohusika na masuala ya uwekezaji kuchangamkia fursa hiyo.
Aidha, Waziri Mkuu alisema licha ya Tanzania kuwa na maeneo
na mazingira mazuri ya uwekezaji pia ina vivutio vingi vya utalii hivyo,
aliwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara, pia Mheshimiwa Majaliwa
aliyakaribisha makampuni na mawakala wa utalii waje nchini na kuwekeza katika
ujenzi wa hoteli za kitalii katika miji mbalimbali yakiwemo majiji ya Dar es
Salaam, Mwanza na Dodoma.
Mheshimiwa Majaliwa alisema kwa sasa Serikali inaendelea
kuimarisha miundombinu ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, barabara, viwanja vya
ndege na nishati ya uhakika ili kurahisisha shughuli mbalimbali zikiwemo za
uwekezaji.
SHAMBA LA MIFUGO MILAN
Sekta ya Mifugo ni moja ya eneo ambalo Serikali ya awamu ya
sita imeweka msisitizo wa kuhakikisha inakuwa ili kuwanufaisha wafugaji nchini
kwa kuwafanya kufuga kisasa na kuondokana na ufugaji usio na tija.
Dhamira hii ilimfikisha Mheshimiwa Majaliwa katika moja ya
shamba la mifugo mjini Milan nchini Italia ambapo Oktoba 19, 2023 alitembelea
shamba la ufugaji wa ng'ombe wa maziwa la Alesandra linaloendeshwa kwa kutumia
mifumo ya kisasa ya kielektoniki ikiwemo ukamuaji wa maziwa kwa kutumia roboti.
Akiwa katika shamba hilo lenye takribani ng'ombe 500,
Mheshimiwa Majaliwa alishuhudia mifumo bora ya ufugaji, ulishaji, unyonyeshaji
na ukamuaji wa maziwa, ambapo ng'ombe mmoja anauwezo wa kutoa lita kuanzia 35
hadi 70 kwa siku na kumuwezesha mfugaji kupata tija zaidi.
Aidha, Waziri Mkuu alitoa wito kwa wafugaji nchini wakubali
kubadilika na wafuge kwa kutumia teknolijia ya kisasa ili wanufaike zaidi na
shughuli hiyo. “Tubadilike tupate manufaa zaidi, ufugaji ni uchumi, ufugaji ni
maisha na ufugaji ni kazi, hivyo tubadili mfumo wa ufugaji wetu kwa ajili ya
kujiongezea kipato zaidi.”
Naye, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamata Shaame Hamisi alisema amefurahishwa
na misingi bora ya ufugaji na kwamba utaratibu huo ukitumika nchini utaongeza
tija katika sekta ya mifugo.
Alisema aina ya ufugaji inayotumika kwenye shamba hilo
kuanzia hatua uandaaji wa malisho, ukamuaji wa maziwa, usafirishaji na utunzaji
wa mifugo aliojifunza shambani hapo atakwenda kuufanyia kazi kwa lengo la
kuimarisha sekta ya mifugo ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato kwa wafugaji na
Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde
alisema amefurahishwa na namna ya uendeshaji katika shamba hilo ambalo pia
wanafanya kilimo mseto kwa kufuga, kulima malisho ya mifugo na kutumia kinyesi
cha ng'ombe kuzalisha nishati ambayo wanaitumia kwa shughuli za shambani na
ziada kuuza kwenye gridi ya Taifa.
Alisema jambo jingine lililomfurahisha katika shamba hilo ni
namna ambavyo mifugo yao imewekewa hereni za kielektroniki kwa ajili ya
utambuzi ambazo zinaiwezesha nchini kujua idadi ya ng'ombe pamoja na maendeleo
yake ikiwemo kutambua magonjwa, hivyo atakutana viongozi wa sekta husika ili
kuangalia namna bora ya kuboresha ufugaji nchini.
Naye, mfugaji wa ng'ombe kutoka Wami Sokoine, Morogoro,
Mainga Ole Kalaita ambaye alitembelea shamba hilo kwa ajili ya kujifunza
ufugaji bora alisema amepata elimu ya ufugaji bora na atakwenda kuwashauri
wafugaji wenzake nchini wabadilike ili waendane na mahitaji ya sasa ya soko
ikiwa ni pamoja na kubadili njia za ufugaji. “Hakuna haja ya kuwa na mifugo
mingi isiyokuwa na tija, tubadilike tufuge kisasa.”
Ole Kalaita alisema kuwa kuna haja ya wafugaji nchini
kukubali mifugo iwekewe hereni kwa ajili ya utambuzi wa aina ya uzao wa ngombe
kwani katika masoko ya kimataifa lazima wahoji historia ya mfugo, aliiomba
Serikali iendelee kuwaelimisha wafugaji umuhimu wa kuwa na taarifa za mifugo.
Awali, mmiliki wa shamba hilo, Bibi Alessandra Soresina
alisema katika shamba hilo wanatumia teknolojia ya uhimilishaji wa mifugo kwa
lengo la kuwa na kosafu za mifugo yao. Teknolojia hiyo inawasaidia kuwa na
uhakika wa kuwa na muendelezo mzuri wa ng'ombe wanaotoa maziwa kwa wingi.
“Wakati mwingine hutumia akili bandia ili kuweza kubaini mbegu za ngombe jike
pekee kwa ajili ya uhimilishaji ila njia hii hugharimu fedha nyingi zaidi.”
Alisema ng'ombe wote wanapewa chakula kinachozalishwa
shambani hapo kwa kuchanganya mahindi na nyasi zilizohifadhiwa vizuri kwa kutumia
teknolojia ya kisasa na mifugo hiyo inapewa chakula mara tatu kwa siku ambapo
ratiba hiyo inaweza kubadilika kulingana na msimu. Kwenye shamba hilo hakuna madume
na iwapo ikitokea ng'ombe amezaa ndama dume, ndama hao huuzwa.
Aliongeza kuwa ng'ombe wao wamevalishwa hereni ikiwa ni
utambulisho rasmi unaohusisha aina, uzao, asili, utambuzi wa mmiliki na
kuwezesha ufuatiliaji wa maendeleo yake ikiwemo kutambua magonjwa, uwezo wa
kutoa maziwa pamoja na kujua kama anakula vizuri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya
Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa alisema mamlaka yao imefaidika sana kwa
kushiriki katika jukwaa hilo kwa sababu sekta zote walizozitangaza zikiwemo za
ujenzi, viwanda zimeonesha kufurahiwa na wadau wa uwekezaji, hivyo wamejipanga
kupokea wafanyabiashara.
Awali, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mheshimiwa Balozi
Mahmoud Thabit Kombo amemshukuru Mheshimiwa Majaliwa kwa kushiriki katika
jukwaa hilo na kwamba ofisi hizo za Ubalozi wa Tanzania nchini Italia zitatoa
ushirikiano kwa wafanyabiashara na wawekezaji wote waliokuwa tayari kuja
kuwekeza na kufanya biashara nchini.
0 Maoni