Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, amewataka Wahitimu wa Mafunzo ya
awali ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwenda kuzuia na kupambana na tatizo la rushwa
kwenye miradi mikubwa ya kijamii inayoendelea kutekelezwa sehemu mbalimbali
nchini kwani Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
hiyo.
Mhe. Simbachawene amesema Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha maisha ya
Watanzania yanakuwa bora zaidi kwa kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ikiwemo elimu, afya pamoja na maji inatumika kwa malengo
yaliyokusudiwa na sio kuingia katika mifuko ya watu wachache.
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo wakati wa hafla ya
kufunga Mafunzo ya awali kwa Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi 370 wa
TAKUKURU yaliyofanyika katika Shule ya Polisi Tanzania mjini Moshi, mkoani
Kilimanjaro.
Mhe. Simbachawene amesema, maono na malengo ya Serikali ni
kuhakikisha wahitimu hao wanakwenda kuzuia rushwa na ikishindikana kuzuia wakapambane
nayo kwani rushwa inapofusha na ni ukosefu wa ustaarabu katika jamii.
“Kazi yenu kuu sio kupambana na rushwa bali kuzuia kabla
haijatokea na ndio maana Serikali imeamua kuajiri watumishi wa taaluma
mbalimbali wakiwemo Maafisa Ununuzi, Wahasibu, Wasanifu majengo na wataalamu wa
TEHAMA ili mkawe mbele katika kuzuia kulingana na taaluma zenu na kushauri
ipasavyo mnapoona kuna dalili za rushwa’’ amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Katika hatua nyingine Mhe. Simbachawene ametoa rai kwa
wahitimu hao wa TAKUKURU kutulia katika vituo vya kazi watavyopangiwa na
kuachana na mawazo ya kuhamia sehemu nyingine kwa madai ya kutafuta masilahi
zaidi.
“Wenye mawazo ya kuwa hapa TAKUKURU mnapita tu naomba
niwaambie ukweli, hakuna kitu kama hicho, ninyi mmepewa mafunzo maalum kwa
manufaa ya kuwahudumia Watanzania kupitia TAKUKURU na sio kuhamia katika vituo
vingine vya kazi,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP Salum Hamduni amesema
ajira hizo kwa wahitimu hao zilikuwa ni za kimkakati lengo likiwa ni
kuhakikisha maeneo yaliyokuwa hayawezi kufikiwa na TAKUKURU yanafikiwa kwa sasa
na kwa urahisi zaidi.
‘’Mhe. Waziri hawa wahitimu unawaona wengi wao ni Maafisa
ambao ni wahitimu katika vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini katika maeneo
tofauti wakiwemo Mainjinia lengo letu ni kuhakikisha mianya yote ya rushwa inadhibitiwa,
CP Hamduni ameongeza.’’
Mafunzo haya ambayo ni takwa la kisheria kwa kila mtumishi
anayeajiriwa TAKUKURU yamefanyika kwa muda wa miezi mitano kwa Maafisa
Uchunguzi na miezi mitatu kwa Wachunguzi Wasaidizi.
Na. Lusungu Helela-Moshi
0 Maoni