MKURUGENZI MKUU wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na
Kilimo (FAO) Dkt. Qu Dongyu amesema kuwa Shirika hilo limevutiwa na mradi wa
kuwawezesha vijana unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania wa Jenga Kesho
Iliyobora “Building Better Tomorrow” (BBT).
“FAO tutaunga mkono mradi huu ili Serikali ya Tanzania iweze
kutimiza malengo ya kuwainua vijana na wanawake kwenye sekta ya kilimo kama
ilivyo moja ya agenda kwenye mkutano wa FAO wa mwaka 2023”.
Ameyasema hayo Jumatano alipokutana
na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ofisi za Makao
Makuu ya FAO zilizopo Rome, Italia. Waziri Mkuu yuko nchini Italia
akimuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa
Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023.
Aidha, Mkurugenzi huyo amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza sekta ya kilimo pamoja na kuboresha
mahusiano na mashiriki ya kimataifa.
Dkt. Dongyu ameahidi kutembelea Tanzania mwaka 2024 kwa
ajili ya kujionea maendeleo katika sekta ya kilimo pamoja na kupanua wigo wa
majadiliano kati ya Tanzania na Shirika hilo ili kuendelea kuwezesha zaidi
sekta ya kilimo na uchumi wa Buluu.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu alisema kwa sasa Serikali ya
Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanza
kupanua wigo wa kilimo kutoka cha kutegemea mvua na kujikita zaidi kwenye
kilimo cha umwagiliaji, ambapo imetenga shilingi bilioni 900.
“Kilimo ndio maisha, kilimo ndio chakula, tunataka kujikita
zaidi katika kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia mabwawa yetu/ Tunataka
tujiridhishe kuwa hakuna Mtanzania atayekufa kwa kukosa chakula.”
Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali inaendelea kufanya
maboresho katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo na kuhakikisha kinasimamiwa
kwa kiwango cha juu ili kuzalisha chakula cha kutosha kwa matumizi ya ndani na
ziada kuuza nje.
Kadhalika, Waziri Mkuu alisema kuwa mbali na maboresho hayo
yaliyofanyika katika sekta ya kilimo, pia Serikali inawasimia wakulima kuanzia
hatua za awali za maandalizi ya mashamba hadi kwenye utafutaji wa masoko
kupitia maafisa ugani ambao wapo hadi vijijini.
Pia, Waziri Mkuu Alisema Serikali imeanza kusajili wakulima
katika mfumo wa kidigitali lengo ni kujua idadi ya wakulima, ukubwa wa mashamba
pamoja na aina ya mazao wanayolima ili kurahisisha ufikishwaji wa huduma za
ugani kwa wakati zikiwemo pembejeo. “Usajili huo hautaishia kwa wakulima pekee
bado utaendelea hadi kwa wavuvi, wafugaji pamoja na watumiaji wote wa ardhi.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa alitumia fursa
hiyo kuishukuru FAO kwa uamuzi wake wa kuiunga mkono Serikali ya Tanzania
katika utekelezaji wa mpango wa BBT ambao unalenga kuwawezesha vijana na
wanawake kushiriki katika kilimo chenye tija.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni