Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imesema kuwa inaandaa
Kanuni mahususi kwa ajili ya kusimamia ununuzi wa tiketi za abiria kwa njia ya
mtandao ikiwa ni pamoja na kuweka masharti kwa watoa huduma wa mifumo ya Tiketi
Mtandao.
Hayo yameelezwa leo Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa
LATRA CPA Habibu Suluo wakati akiongea na Wahariri wa vyombo vya habari, katika
mwendelezo wa mikutano ya taasisi za umma inayoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa
Hazina.
“Mabasi yote ya masafa marefu yameunganishwa na mfumo wa
Tiketi Mtandao na kwa kiasi kikubwa mfumo huo umesaidia kudhibiti upandishaji
holela wa nauli, lakini ili kuwa na usimamizi mzuri tunaanda Kanuni za kusimamia
eneo hilo,” alisema CPA Suluo.
Pia, amesema kwamba mamlaka imeandaa mfumo tumizi wa LATRA
unaopatikana ‘Play Store’ kwenye simu zote za Android ili kumwezesha mwananchi
kupata taarifa za nauli za mabasi ya masafa marefu na mabasi ya mijini.
CPA Suluo ameongeza kwamba kwa sasa Mamlaka ya Udhibiti
Usafiri Ardhini (LATRA) inaendelea kuboresha huduma za mfumo tumizi
wa LATRA ili kuwezesha abiria kutambua mwendo kasi wa gari.
Akizungumzia mapato ya LATRA, amesema katika kipindi cha
mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2021/22, mapato ya Mamlaka yaliongezeka kutoka
Shilingi Bilioni 25.945 hadi Shilingi Bilioni 28.53 ikiwa ni ongezeko la Shilingi
Bilioni 2.58 sawa na ongezeko la 10%.
Aidha, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 hadi
2022/23, mapato ya Mamlaka yaliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 28.53 hadi
Shilingi Bilioni 34.17 (kabla ya kukaguliwa na CAG) ikiwa ni ongezeko la
Shilingi Bilioni 5.64 sawa na ongezeko la 20%.
CPA Suluo amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya
utekelezaji wa majukumu ya LATRA, mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2022/23, mapato
ya Mamlaka yaliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 25.95 hadi Shilingi Bilioni
34.17 (kabla ya kukaguliwa na CAG) ikiwa ni ongezeko la Shilingi Bilioni 8.22
sawa na ongezeko la 32%.
Kwa upande wa utoaji wa leseni kwa vyombo vya biashara CPA
Suluo amesema katika kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2022/23, idadi ya leseni za
usafirishaji ziliongezeka kutoka 230,253 hadi 284,158 sawa na ongezeko la
leseni 44,205 ambayo ni ongezeko la asilimia 18.4.
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilianzishwa kwa
Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura 413 ili kudhibiti huduma za
usafiri ardhini katika Sekta za Reli, Barabara na Waya.
0 Maoni