Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika
kuongeza mazao mapya ya utalii, hivi karibuni wamegundua eneo jipya lenye
hazina kubwa ya Nguzo za Asili (Natural Pillars) zenye muonekano wa kuvutia
ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha.
Nguzo hizi zilizosimama mithili ya uyoga na kuvutia kwa
macho zinasemekana zimetokana na kulika (kumomonyoka) kwa miamba yenye sifa
tofauti kunakosababishwa na mwenendo mzima wa mtiririko wa maji na wakati
mwingine pia zikichagizwa na upepo.
Kwa muonekano wa nguzo hizi na jinsi zilivyopangika utadhani
kuna Mhandisi kazitengeneza na kuzinakshi, cha kustaajabisha zaidi tabaka la
juu lina mwamba mgumu mithili ya kichwa cha binadamu na chini ni kama
zimeshikiliwa na mizizi zisianguke, chini ya nguzo hizo pia kuna utitiri wa nguzo
ndogo ndogo zinazoendelea kumea na kuongezeka kimo kadri siku zinavyoendelea.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Godwell Meing’ataki, Mkuu wa
Hifadhi ya Taifa Ruaha alisema, "Kwa mara ya kwanza tukiwa tunashuka na
Helikopta katika eneo hili, tulishangazwa na wingi wa nguzo hizi za asili
(Natural Pillars) na tukajua ndio hazina pekee iliyopo hapo, lakini
tulipolizunguka eneo hili tuligundua lina utajiri mwingine wa masalia ya Zana
za Mawe mithili ya zile zilizotumika nyakati za Zama za Mawe za Mwanzo."
Zana zinazoonekana katika eneo hilo jipya ni pamoja na mawe
magumu yaliyotumiwa na binadamu wa mwanzo kusagia nafaka kwa ajili ya chakula
au mizizi na magome ya miti kwa ajili ya tiba asilia, miamba iliyochongwa
kiustadi mithili ya mikuki, mashoka na zana nyingine zilizotumika katika
shughuli za uwindaji.
Kwa mgeni mwenye kumbukumbu na ufahamu wa Nguzo za Asili
(Natural Pillars) na zana za mawe zilizopo Tanzania anaweza kusema hapo ni
Isimila, la hasha! ni moja ya eneo lililopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha takribani
kilometa 70 kutoka Makao Makuu ya hifadhi hiyo yaliyopo Msembe.
Aidha, Kamishna Meing'ataki alisema, “Kwa utajiri wa nguzo,
zana za mawe pamoja na sifa nyingine kedekede eneo hili linakidhi vigezo vya
kuwa Geopark, kama tunavyofahamu Bara letu la Afrika lina Geopark mbili tu
lakini tunashukuru ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha tuna eneo linaloweza kukidhi
vigezo hivyo, likikidhi vigezo litatoa fursa kwa hifadhi hii kutambulika zaidi
kimataifa tofauti na ilivyo sasa."
Jitihada za kulitangaza eneo hili zimeanza ndani na nje ya
mipaka ya Tanzania ili kuvutia watalii wengi zaidi na wawekezaji, ukizingatia
kuwa hiki ni kivutio kipya na muhimu kwa watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa
Ruaha na hifadhi nyingine zilizoko Ukanda huu wa Kusini.
Kamishna Meing'ataki alisema, "Shirika la Hifadhi za
Taifa Tanzania (TANAPA) litafanya taratibu za kuwaalika watafiti mbalimbali wa
miamba, udongo na Malikale (Archiolojia) wa ndani na nje kubaini na kupata
taarifa sahihi za malikale zilizopo, taarifa ambazo zitalitambulisha eneo hili
kimataifa".
Aidha, kutokana na unyeti wa eneo hili Menejimenti ya
Hifadhi ya Taifa Ruaha imefanya jitihada za kutengeneza barabara ili eneo hilo
lifikike kiurahisi hasa kipindi hiki ambacho watalii wengi wanashauku na
bashasha ya kwenda kulitembelea na kuziona nguzo na zana hizo.
"Uimarishaji wa barabara unaenda sambamba na tathmini
za kiutalii, kiikolojia na kiulinzi kubaini maeneo muhimu yatakayojengwa
miundombinu ya kiutalii ili wageni wanapolitembelea eneo hilo wapate huduma ya
malazi na chakula. Hatua hizi zikikamilika zitavutia watalii wengi na siku za
kukaa hifadhini zinatarajia kuongezaka, siku zikiongezeka na mapato
yanaongezeka kwa taifa," alisema Meing’ataki.
Eneo hilo limegunduliwa na Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa
Ruaha na kupewa jina la "Ruaha Magic Site" tofauti na hapo awali
lilikuwa likijulikana kama "Magda", "Ruaha Magic Site"
inasadifu zana nzima ya utalii.
Na. Jacob Kasiri - Ruaha
0 Maoni