WAZIRI MKUU Mhe. Kassim Majaliwa amesema Shirika la Umoja wa
Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) limeahidi kuunga mkono jitihada za Serikali
ya Tanzania katika kukuza na kuendeleza sekta ya kilimo.
Mhe. Majaliwa Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zina mipango ya kuifanya Tanzania
kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula ndani ya nchi na ziada kuuza nje ifikapo
2030.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana jioni (Jumatatu, Oktoba 16,
2023) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani
ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023. Waziri Mkuu amehutubia mkutano huo kwa
niaba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kabla ya ufunguzi wa mkutano huo uliowahusisha Wakuu wa nchi
na Serikali, Waziri Mkuu alishiriki katika Maadhimisho ya miaka 78 tangu
kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).
"Pamoja na jitihada ambazo tumeziweka ndani za
kushirikisha vijana na wanawake kuhakikisha kwamba tunaongeza teknolojia,
kutumia mbolea kwenye kilimo, pamoja na ushirikishaji wa sekta binafsi,
tumeamua kuungana na FAO kupitia Mkurugenzi Mkuu na wameahidi kutuunga mkono
kwenye Sekta ya kilimo."
Amesema Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu
mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, barabara na nishati vijijini ili
kurahisisha shughuli za kilimo. “Maboresho mengine ni ujenzi wa viwanda vya
kuzalisha pembejeo za kilimo na kuhamasisha wakulima kutumia teknolojia za
kisasa katika uzalishaji.”
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Dkt. Qu Dongyu
amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kuendeleza sekta ya kilimo na uchumi wa
buluu, hivyo Shirika lao liko tayari kushirikiana na Tanzania katika kutoa
msaada wa kitaalam pamoja na kukuza mifumo ya uzalishaji wa chakula.
Naye, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamata Shaame Hamisi alisema kwa sasa
Serikali inafanya maboresho makubwa katika sekta ya kilimo na miongoni mwa
maboresho hayo ni utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji ambayo inalenga
kuimarisha upatikanaji wa chakula.
Awali, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema
Serikali imeendelea kuwashawishi vijana kushiriki katika shughuli za kilimo
kwani mbali na kuongeza uzalishaji wa chakula, pia kilimo ni miongoni mwa sekta
zinazotoa ajira nyingi, hivyo watakuwa wamejihakikishia ajira.
Mkutano huo ulifunguliwa na Rais wa Italia Mhe. Sergio
Mattarella na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Ireland Mhe.
Michael Higgine, Rais wa Iraq Mhe. Abdul Latif Rashid, Mfalme wa Lesotho,
Viongozi wa Ujumbe kutoka Nchi Wanachama, Viongozi Wakuu wa Mashirika ya Umoja
wa Mataifa (FAO, IFAD & WFP).
Na. Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni