Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amevitaka vyama vinavyoshughulika na masuala
ya wazee nchini kufanya kazi kwa karibu na Mabaraza ya kisera ya Wazee kupitia
mwongozo wa Kitaifa uliozinduliwa tarehe 6 Oktoba 2023 kwenye Maadhimisho ya
Siku ya Wazee kitaifa mkoani Geita.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Chama cha Wazee
Wanaume Tanzania iliyofanyika jijini Dodoma leo Oktoba 27, 2023, Waziri Dkt.
Gwajima pia amesisitiza Asasi na Vyama vyote vya Wazee nchini kutekeleza
majukumu yao kwa mujibu wa Sera, Sheria, Miongozo na Mipango ya Serikali huku
wakizingatia Katiba zao bila kuingilia majukumu ya mamlaka nyingine au vyama
vingine pamoja na kuwa na mikakati ya kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza
shughuli zao kikamilifu.
Kuhusu kudhibiti mmomonyoko wa maadili Waziri Dkt Gwajima
amesema, Chama hicho pia kina wajibu wa kuchochea Malezi chanya ya Watoto na
Vijana, huku wajumbe wa Chama hicho wakiwa mfano kwenye kuwajibika kukemea
mmomonyoko wa maadili katika jamii unaosababishwa na kukosa malezi stahiki.
Ameziahidi Asasi na vyama vyote vya Wazee kuwa, Serikali
itaendelea kuwapa ushirikiano ambapo amezitaja baadhi ya juhudi zinazofanywa na
Serikali kuwa ni pamoja na Kuunda mabaraza ya ushauri wa masuala ya wazee
ambayo ni kiungo cha kisera kati ya jamii ya wazee wa makundi mbalimbali na
Serikali.
Aidha, kwa kushirikiana na majukwaa ya wazee serikali
imeweza kufanya mapitio ya Sera ya wazee ya mwaka 2003 na kuja na rasimu ya
sera mpya ya wazee ya mwaka 2023 ambayo iko kwenye hatua za mwisho.
Akitoa salaam za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya
Chemba Mhe. Gerard Mongela amewataka wazee kuwa sehemu ya kusaidia maendeleo ya
nchi kwa kuendelea kuwa washauri wazuri na kuwafungulia mlango vijana
wanaotumikia taifa.
"Viongozi vijana wanahitaji sana hekima ya wazee, chini
ya Uongozi wa Rais Samia mkawe kielelezo, muendelee kutoa ushauri bila kuchoka.
Kupitia Chombo chenu, mtumie taaluma zenu muweke kwenye maandishi ili iwe
kumbukumbu," amesema Mhe. Mongela.
Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Taifa wa Chama
cha Wazee Wanaume Joseph Laizer amebainisha kwamba Chama hicho kimetokana na
kuwa na malalamiko mengi ya kusahaulika kwa wazee hasa katika huduma za afya na
maadili.
"Tumeamua kurudi kule tulipotoka, tujaribu kurudisha
maadili vijijini, watoto wetu wanaposoma wanabadilika na kusahau jadi yao"
amesema Laizer
Kwa upande wake Katibu Mwenenzi wa Chama cha Wazee Wanaume
John Sagata akiwasilisha risala ya chama hicho amesema lengo la chama hicho ni
kuungana wanaume wazee katika kujadili masuala yanayowahusu ambapo hadi sasa
kina jumla ya wanachama 23146 katika mikoa 22 nchini.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dodoma Mchungaji
Paulo Mpolo amebainisha kuwa, Baraza la Wazee ndio linabeba wazee wote wa kike
na wa kiume hivyo amekiomba chama cha Wazee na
vyama vingine vyote kushirikiana katika kuwatetea wazee.
"Kazi ya kutengeneza malezi na maadili yoyote ni kazi
ya wazee, tulijisahau tukaacha kuwasaidia watoto wetu juu ya maadili yetu ya Kiafrika. Tuamke sasa
na tukatae kuitwa tumepitwa na wakati, tusaidie kizazi chetu." amesema
Mzee Mpolo.
Na. WMJJWM- Dodoma
0 Maoni